09/08/2017

Urithi uliopotea Afrika (2) : duma

Tanbihi : makala hizi zote katika mlolongo huu « urithi uliopotea Afrika » zimeandikwa mwaka 2017 ili zisomwe mwaka 2050. Maudhui yote yanaambatana na mazingira ya Afrika na wanyamapori wake. Inachukuliwa bayana kwamba viumbe wote wale ambao wanagusiwa katika makala hizi wamepotea. Sababu zisizopingika zinafamahika wazi, nazo ni uharibifu wa mazingira pamoja na ongezeko la watu bara la Afrika. Picha zote penye ukurasa huu ni zangu. 

---------------------------------


Zamani duma (Acinonyx jubatus) walivuma sana katika mbuga zote za Afrika. Duma ni mnyama aliyetambulika duniani kwa kuwa na mwendo wa upesi wakati wa kukimbia (hadi km 115 kwa saa). Alikuwa hukimbia kama mshale katika nyanda za mbuga. Ni sifa yake maarufu. Katika nduni nyingine za ajabu ambazo zilimfanya awe mwindaji hodari, mnyama huyo alikuwa na uti wa mgongo napukivu (flexible) na mkia mrefu ambazo zilimsaidia apate ufanisi mkubwa katika kusaka wanyama wengine. Uti wa mgongo wake ulikuwa unanyumbulika kwa kiasi fulani, jambo ambalo lilichangia pia katika kuotea mawindo wake na kuwakimbiza. Mkia wake pia ulikuwa unatumika kama usukani wa kumsaidia ajipatie mizani wakati wa kukimbia. Kwenye video ya chini tunaona vizuri jinsi alivyoutumia. Kucha zake pia zilikuwa hazifutiki kabisa kwenye mguu wake (uliokuwa mgumu zaidi kuliko paka wengine) na zilifanana zaidi na zile za mbwa kuliko paka. Kazi zake zilikuwa na ufanisi mwingi kwa kuongeza mashiko yake chini na kukamatia udongo anapokimbia. Vipengele hivi vyote vilimsaidia kukimbia upesi wakati wa kuwinda au wakati wa kukwepa maadui wake ambao walikuwa wengi porini, wakiwemo simba, chui, fisi na mbwa msitu (nisitaje mnyama mwenye miguu miwili anayejitia utamaduni mwingi).

                         
  
Mnyama huyo alikuwa ni mgwizi (alikula nyama ya wanyama wengine). Mawindo yake yalihusisha wanyama wengi wa porini wasiozidi kilo 60, wakiwemo swala pala, swala tomi na granti, sungura na wanyama wengi wadogo. Wanyama hawa wote wanapatikana siku hizi katika zoo kadhaa, hasa Ulaya na Amerika kaskazini. Kama duma, wameteketea vibaya kwa kukosa nafasi na makao ya kuishi. Duma jike ndiye wa pekee katika familia ya paka ambaye huweka mipaka katika eneo lake alilolitawala huku akilitetea dhidi ya majike wengine. Duma dume naye huranda huku akitafuta jike mwenye dalili ya kujamiana. Kwa kawaida familia ya duma huwa ya mzazi mmoja, kwani duma jike ndiye anayewatunza watoto. Hapo tena ni mfumo wa kijamii usiokuwa na kifani katika jamii ya paka kwa jumla. Duma dume nao walikuwa huishi pamoja kwa kupendeleana, nao ushirikiano huo ulikuwa una dhima fulani katika kujihami na kujitetea dhidi ya wabuai (predators) waliokuwa huwinda wabuawa (preys) wamoja.

                             

Watu wachache wanajua kwamba alikuwa ni mdhaifu mno kutokana na muundo wake wa chembe za urithi. Sio kwa sababu alikuwa amedhoofika kutokana na umbo lake, kwa kuonyesha sura nyonge. Na kweli alikuwa na miguu mirefu na gimba la mwili wake lilionekana jembamba sana. Mbali na hayo, kijenetikia alikuwa ni mnyama mpungufu na mpweke katika jenera Acinonyx. Hiyo ndiyo sababu alikuwa mdhaifu. Nduni hiyo ya kipekee ya kutokuwa na chembe nyingi za urithi zilizotofautiana ndiyo iliyomtambulisha miongoni mwa paka wote wa duniani, kabla ya kuangamia. Kiwango fulani cha chembe za urithi kinatakiwa katika maumbile ya viumbehai ili kustahimili mabadiliko ya mazingira au kukabili shinikizo nyingine, mathalan maradhi na maambukizo ya kujitokezea. Ongezeko hobela hobela la watu duniani pamoja na ustawi wa mfumo wa kiuchumi unaoathiri sana mazingira asiliya ya duma (pamoja na viumbehai wote) huleta hali ya msukosuko ambayo huvuruga makazi yake.

Uchunguzi wa ziada uliofanywa na wana sayansi kadha unaaridhia kwamba udhaifu huo ulikuwa na sababu zake. Msomaji ukiangalia ramani hiyo ifuatayo utaona kwamba awali duma alikuwa akiishi katika eneo kubwa la duniani, si Afrika pekee, bali hata sehemu kadhaa za Asia. Alitoweka kabisa kwa sababu mbili : kwanza katika historia ndefu ya mnyama huyo (muda wa miaka takriban milioni 3), ilitokezea mageuko katika spishi yenyewe kutokana na uteuzi asiliya, mchakato ambao ulisababisha spishi hii ya duma kujenga maumbile hafifu isiyokuwa na kingamwili nyingi mwilini mwake. Tukio hilo lilitokezea miaka 12 000 nyuma, wakati tabia ya dunia ilipobadilika ikawa asimilia 75 ya wanyama wa aina mbalimbali — hasa mamalia — wakatoweka kwa kushindwa kubadilika kulingana na hali mpya katika mazingira. Duma wale walionusurika kutoka katika uangamizi huo mkubwa waliondokea wamepungukiwa kiasi fulani katika maumbile yao, ikawa spishi hiyo ikaonyesha muundo sawa wa chembe za urithi, kitu ambacho kilimdhoofisha. Pili, mnyama huyo, ambaye alikuwa si mkali sana wa kuweza kushambulia binadamu na kuathiri uchumi na maslahi zake, aliwahiwa kukutana na kupambana na wanadamu ambao walimweka mikazo na shinikizo nyingi sana.Maeneo yake kwanza yakapungua sana akafukuzwa kutoka katika sehemu nyingi alikokuwa akiishi tangu zamani. Na hasa Afrika ambapo watu kwa jumla hawapendi wanyamapori, matokeo yake duma wengi walipotea wakabaki vikundi vikundi kwanza (hadi miaka 2025-2030) kisha wakatoweka daima dawama. Mchakato huo wa uharibifu ulimkumba vibaya kwa sababu mbili : kwanza watu walimsaka vibaya huku wakichukua makao yake ya kuishi ; pili, kutokana na hali yake kijenetikia, mnyama huyo alidhurika sana alipolazimishwa kuishi karibu na binadamu. Wengi walikufa kwa sababu ya maradhi nyingi zilizoletwa na wanadamu na mifugo yao, mathalan ugonjwa wa kimeta. Aidha, kutokana na hali yake asiliya ya kuwa chembe za urithi za aina moja, duma alianza kukabiliwa na utasa kwa wengi sana, jambo ambalo lilipunguza fursa ya kuweza kutunga mimba na kupata watoto. Nisitaje pia mabadiliko ya makazi ya asili ambayo yalikithiri sana wakati ongezeko la watu bara ya Afrika lilaangamiza kila kitu huku yakighasi tabia na mienendo yake yakahujumu mustakabali wake.
Kitambulisho :

Uzito — jike : kg 21-42. Dume : kg 36-72.
Cheo hadi mabega — jike : sm 65-81. Dume : sm 79-94.
Urefu — jike : m 1.10 – 1.30. Dume : m. 1.30 – 1.50. Mkia : sm. 65-85.


LA ZIADA :

Kuhusu duma wa Kenya (Maasai Mara na Meru) : HAPA

The global decline of Cheetah Acinonyx jubatus and what it means for conservation : HAPA.

Cheetah Conservation Fund : HAPA


                                            

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni