25/08/2017

Urithi uliopotea Afrika (3) : simba


Tanbihi : makala hizi zote katika mlolongo huu « urithi uliopotea Afrika » zimeandikwa mwaka 2017 ili zisomwe mwaka 2050. Maudhui yote yanaambatana na mazingira ya Afrika na wanyamapori wake. Inachukuliwa bayana kwamba viumbe wote wale ambao wanagusiwa katika makala hizi wamepotea. Sababu zisizopingika zinafamahika wazi, nazo ni uharibifu wa mazingira pamoja na ongezeko la watu bara la Afrika. Picha zote penye ukurasa huu ni zangu. 

---------------------------------

Ni kicheko cha dhihaka na pia aibu kwa binadamu kuona kwamba hakuna nchi ya Afrika isiyokuwa na timu yake ya mpira yenye jina « Simba », wakati simba wenyewe wa porini wametoweka kabisa. Hakuna tena. Wote wamefutiliwa mbali. Sumu, mkuki, mitego ya waya, bunduki, panga, mawe, mishale, bombomu na kadhalika, mbinu za kila aina zilitumika ili kuwamaliza. Wamebaki wachache tu, katika nchi za magharibi, kunako hifadhi ya aina ya zoo. Huko wataalamu wanajitahidi kuwatunza ili spishi hii isitoweke kabisa. Lakini majangili wangali wanakwenda Ulaya ili kuwasaka ndani ya zoo ili wajipatie hirizi zao.

Simba (Panthera leo) alikuwa ni mnyama aliyezagaa sana bara ya Afrika na kwingineko, mathalan Asia. Alipatikana katika mazingira mbalimbali kutoka maeneo ya savana, nyika zenye vichaka vidogo vidogo hadi kando za misitu ya mvua ama maeneo yenye ukame mwingi kama vile jangwa zenye vipori vidogo na viotea vya muda. Muhimu kwake ni kupata maji na mawindo. Alikuwa hapatikani katika milima mirefu ingawa simba wachache walikuwa huishi katika milima ya Bale, Ethiopia, hadi urefu wa mita 3500 juu ya usawa wa bahari. Msomaji ukiangalia ramani iliyopo chini, utakuta kwamba simba alikuwa huishi kila sehemu ya Afrika isipokuwa katika mabonde ya misitu mikubwa ya Kongo na katika jangwa la Sahara. Ramani hiyo inaonyesha usambazaji wake mwaka 2015. Leo hii mwaka 2050, wote wamepotea.Simba alikuwa ni mnyama aliyekuwa huishi kiujamaa. Katika mbari wa paka ukusanyao chui, simbamangu, duma, mondo na wengineo, alikuwa ni mgwizi pekee aliyeishi kikundi. Mfumo huu wa kijamii ulivutia sana wana sayansi na utafiti mwingi ulifanyika wakati alikuwa huishi porini. Simba walikuwa huishi pamoja kwa vikundi vikundi, na aghalabu tuliwakuta wakigawanyika vikundi viwili. Kimoja kilikusanya majike na watoto wao na kikundi kingine kilikuwa kinajumlisha madume wachache, na wakati mwingine dume alikuwa mmoja tu. Kikundi cha madume kilikuwa kikiishi kando ya kile cha majike, si mbali wala si karibu sana. Kikundi cha majike kilijumuisha simba kati ya 4 hadi 12, wakati madume walikuwa kati 1 hadi 6 katika kikundi chao. Ilichukuliwa na wana sayansi kwamba kile kikundi cha majike ndicho kilikuwa msingi wa familia nzima. Sababu ni wazi : majike ndio walioshinda katika kikundi chao hadi kufariki wakati madume wale walikuwa hutoka katika kikundi chao kila baada ya muda wa mwaka moja, huku wakiwa hutafuta sehemu au kikundi kingine kuishi nacho.

                                        

Ndio madume waliokuwa wanaranda, hasa wakiwa bado vijana. Lakini ilikuwa inategemea hali ya uoto waliokuwa wakiishi. Katika nyika ya vichaka vingi, madume huwa waliishi mbali kidogo na majike, huku wakifanya doria katika mizunguko ya pori walipoishi majike ili nao wasifikwe na madume wengine. Familia nzima ya simba ilikuwa huishi katika eneo kubwa kiasi, kutegemea na idadi ya wanyamapori waliokuwa ni mawindo yao. Katika wale wanyama waliokuwa wenye makao pia, kama vile nyamera (topi), kongoni, nyati na swala pala, simba walikuwa hujipatia eneo lisilozidi km 40 za mraba wakati familia nyingine, kama zile zilizoishi katika savana pana zilikuwa hutumia eneo kubwa kiasi cha km 3500 za mraba. Kikubwa hapo ni kukumbuka kwamba familia za simba zilikuwa zinashindana ingawa mapigano makali yalikuwa si mengi. Kila jinsia katika familia ilikuwa na kazi yake : majike walikuwa hukimbiza majike wengine waliokuwa ni wageni, nao madume walikuwa hukimbiza madume wengine wageni. Inamaanisha kwamba kufukuza simba wageni kulikuwa ni kazi ya kushirikiana.

                               .       

Maeneo yote ya simba, au tuseme dola zao, yalikuwa yanathabitiwa barabara kwa kutumia alama ya mkojo na mingurumo ya mawio na machweo. Alama hizo zilikuwa zinatumika ili kuwasiliana na familia au simba wengine. Zilikuwa zinaashiria nia fulani ya kuwepo au kuwasilisha ujumbe fulani kama vile kupata kwa windo. Lakini simba dume alikuwa hangurumi akiwa peke yake katika mizunguko ya kuzurura huku akiwasumbukia simba wengine wenye dalili ya kujamiana. Muhimu hapo ni kujua kwamba mingurumo hii yote ilikuwa ni aina ya kitambulisho kwa kuwa kila simba alikuwa na sauti yake ya kipekee ambayo ilikuwa inamsaidia kutambuliwa na simba wengine. Hapo chini msomaji unaweza kusikia sauti ya jike mmoja niliyewahi kurekodi porini.

                                  .          

Wakati wa joto kali la mchana, simba hao walikuwa hupumzika penye vivuli vya miti na vichaka wakisubiri majira ya magharibi ifike ili waende kuwinda. Simba walikuwa huwinda kila aina ya wanyamapori, wala habagui kama ni mchwa ama ndovu. Alikuwa tayari kumsaka akiwa amehisi kwamba uwezo wa kumpata upo. Akiwa peke yake, alisaka wanyama wa wastani kama swala, ngiri, nyumbu na punda milia. Wakiwa pamoja walishirikiana katika kuwavizia kwanza kisha kuwashambulia. Wataalamu kadha waliwahi kubainisha simba wakisaka kwa mpangilio fulani, huku wakijaribu kupanga kuwinda kwao kwa kutumia mkakati fulani, mathalan wakizingira windo waliolenga ili wamwotee kwa njia rahisi zaidi. Simba mmoja katika kikundi alijihusisha na windo aliyemlenga huku akijaribu kumsukuma kuelekea simba wengine waliokuwa husubiri ng’ambu kumrukia. Huenda kwamba ujuzi huo ulikuwa ni aina ya urithi wa kijamii ama uzoefu uliojengeka katika baadhi ya vikundi kwa kuwa si vikundi vyote vilivyokuwa vinapanga uwindaji wao. Katika vikundi vingine, tuligundua pia kwamba baadhi ya simba walikuwa hujishughulisha na aina ya windo fulani hadi kufika kwenye hatua ya kumteua yule yule kila akimpata katika kundi la mawindo anaowasaka. Tabia hiyo ilichangia sana katika kupata ufanisi katika uwindaji.

                                    .       

Ufanisi katika kuwinda ulitegemea pia hali ya mazingira na jinsi vichaka vilivyokuwa vimesongamana. Katika savana pana, madume walitegemea sana simba majike wa familia yake kwa kuwa walifuga manyoya mengi ushingoni mwao (shungi), kitu ambacho kiliwachongea katika kuwinda. Lakini katika vichaka vingi, vyenye mijiti midogo na manyasi marefu, simba madume walijitegemea kiasi huku wakiwinda kwa kuwashtua na kuwavizia mawindo wake. Tatizo lilitokezea wakati simba dume alipoingia katika uzee, hali ambayo ilimpasa ajitenge na simba wengine aendelee na maisha ya upweke. Simba wengi katika hali hiyo walikufa ama walihangaikia mawindo wadogo wadogo kama vile nungu na ngiri. Simba alikuwa anaweza kula nyama hadi kilo 43 akiwa dume na kilo 22 akiwa jike kutoka kwenye windo mmoja. Hata kama mnyama aliyekamatwa ameuawa na simba jike, simba dume ndiye atakayekula kwanza huku akimsogeza jike kando mpaka ashibe yeye kwanza.

                                              


Simba jike alikuwa anapata joto takriban siku 2 hadi 7 kila baada ya miaka miwili ikiwa amefanikiwa kuwaachisha watoto wake kunyonya. Vinginevyo, kama watoto wake wameuawa hurudi katika hali ya joto baada ya kufa kwa watoto wake. Madume wote katika familia, kama wapo wengi, walikuwa wanamshughulikia jike, lakini mkubwa na mwenye zihi nyingi ndiye aliyekuwa anawapiku wenzake. Mapigo yalitokea mara kwa mara lakini kwa kuwa ni familia moja, yalikuwa ni nadra. Balaa kubwa ilitokezea wakati familia nzima ilikuwa na dume mmoja ambaye nguvu zake zimepungua kwa sababu ya uzee au maradhi. Hapo ndipo simba dume mwingine — ama kikundi cha madume — alipotokea kutoka nje huko akijiingiza katika familia kwa kutumia nguvu na kumfukuza dume mtawala. Mapinduzi hayo yalikuwa yana athari mbaya katika familia kwa kuwa simba dume mgeni, mbali na kumfukuza dume mtawala, alipaswa pia kuwamaliza watoto wadogo wote wa familia ili naye apate nafasi ya kuzaa. Mkakati huo ambao ulikanganya sana akili za wana sayansi ulikuwa una maana yake nzito inayoeleweka wazi tukiwa tunazingatia utaratibu wa uteuzi asiliya. Kwa kuua simba wadogo, huyo simba mgeni anajilazimisha katika kikundi kipya huku akiimarisha chembe za urithi za spishi nzima. Msomaji ukitizama video ifuatayo utaona jinsi simba dume anavyoshambulia familia mpya ili kunyanganya madaraka yote.Kwa nini simba wamepotea ? Zifuatazo ndizo baadhi ya sababu :

kilimo cha binadamu : wakati nchi zote za Afrika zilikuwa na mbuga na hifadhi ili kutunza wanyama pori, hakuna hata moja (isipokuwa Afika kusini, Namibia, na Bostwana) ambayo ilichukua hatua ya kuwachunga na kuwatunza simba. Uhifadhi ulikuwa ni jina tu. Hifadhi zote zilikuwa juu ya « makabrasha ». Katika mizunguko ya hifadhi hizo, wakati idadi ya watu iliongezeka, kilimo kilikithiri na watu wakaanza kuvamia na kunyanganya ardhi ya hifadhi hizo. Kampuni za tasnia ya kilimo pia ambazo mara nyingi zilisajiliwa kutoka nje (kama India, China) zilichangia pakubwa sana katika kunyanganya sehemu kubwa za ardhi zilizokuwa ziko katika dola ya hifadhi. Mifano mingi ipo Ethiopia, Sudan na Tanzania (Selous).

ujangili wa wanyamapori vile vile ulisababisha kupotea kwa simba wengi (mfano Angola). Wakati simba waliponyimwa wanyama waliokuwa huwinda, wengi walianza kutoka katika mbuga na kushambulia binadamu na mifugo yake. Ndipo kulikotokezea maangamizo makubwa sana huku wanadamu wakitumia mitego ya kila aina, hususan mitego ya waya na matumizi ya sumu.

ufisadi na rushwa : wahusika wengi katika kuendesha hifadhi na mbuga za kuwatunza wanyamapori walikubali kupokea rushwa ama hongo za kila aina wakati wachungaji waliomba nafasi ya kuichunga mifugo yao katika malisho mapya, hasa yale ya mbugani.

vita na ukimbizi wa watu : mfano Angola, Kongo, Sudan, Burundi na nchi nyingi za Afrika. Kwa mfano simba wote wa Angola, ambao walichukuliwa na wataalamu wengi ni kundi kubwa imara sana katika idadi ya simba Afrika hadi mwaka 1980, wote waliangamizwa kwa sababu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

maradhi : simba walikuwa ni wanyama wepesi sana katika kuambukizwa maradhi ya pumu iliyoingizwa katika makao yake na mifugo ya binadamu. Aidha, maradhi nyingine kama zile zilizobebwa na vimelea na bakteria ya aina nyingi ziliwapata vibaya sana. Na mchakoto huo mbaya ulikithiri wakati simba walipolazimishwa kuishi ndani ya hifadhi ndogo ndogo kama zile za Uganda, wakadhoofika vibaya kutokana na udhaifu wa chembe za urithi uliowakumba kwa sababu ya kutokutana na simba wengine wa mbali.

uzembe na utepetevu wa hali ya juu katika kuanzisha utafiti na kukusanya takwimu sahihi kuhusu makundi ya simba waliodaiwa walikuwa wengi wakati walikuwa wameshaangamia. Mwaka 1994 ndiko kulikogunduliwa kwamba walibaki simba 20 000 pekee bara nzima ya Afrika, ilhali walikuwa 100 000 mwaka 1980. Nchi zote za Afrika zilipuuza kuanzishwa kwa mikakati ya kutunza simba, na nchi nyingi (kama Tanzania na Burkina Faso) ziliendeleza uwindaji wa kibiashara (au wa kitalii) kama kwamba mambo yalikuwa shwari. Kuhifadhi simba na mazingira yake haikukuwa ni sera yenye kipaumbele katika nchi hizo.

itikadi na imani potovu kuhusu mnyama huyo. Simba wengi, hususan Afrika magharibi, walitegwa wakauawa kwa sababu ya itikadi za kishenzi zinazodai kwamba mkia au meno ya simba zinatibu ukimwi au saratani ya binadamu. Pia katika maoni mengi gundi, mnyama huyo anapachikwa sifa nyingi za kipumbavu, zikiwemo imani za kiuchawi. 


Kitambulisho :

Uzito — jike : kg 110-152. Dume : kg 150-225
Cheo — jike : m 1. Dume : m 1.2
Urefu — jike : m 2.3-2.7. Dume : m 2.5-3.3

Mkia — m 1

La ziada : 

Simba wa Ngorongoro : HAPA
Panthera.org : HAPA
Fences divide lion conservationists : HAPA
Lion Aid : HAPA


Bonyeza picha ujipatie maandishi haya mazuri
Hakuna maoni:

Chapisha Maoni