02/09/2017

Jinsi nchi za Afrika zinavyokubali kutawaliwa kupitia shule za kimataifaSiku hizi kuna njia kadha za kufyonza mali ya nchi na kukandamiza wakazi wake. Njia mojawapo ambayo ni rahisi sana ni kujenga shule ya fahari na kudai kwamba shule hiyo itasomesha wanafunzi kwa kutumia vyombo vya kimataifa. Njia nyingine pia ni kuzorotesha mitaala ya shule za kawaida (ambazo huandikisha watoto wa « wananchi ») ikawa shule hizo zimezuka kiwanda cha kuhamasisha watoto na vijana wasije wakawa watu wazima wenye akili tambuzi ya kuweza kukosoa siasa kandamizi zinazoendesha mataifa. Shule hizo za kimataifa zina nguvu kupindukia za kuweza kumzoesha mtoto akue katika mazingira ambayo yatamleta baadaye katika hali ya kuchukia malezi aliyoyapata nyumbani kwake. Katika shule ya serikali ya Ufaransa nilikofanya kazi mwaka jana hapa Kampala, niliwahi kukutana na watoto wa kiganda walioniajabikia nilipowaambia kwamba ingefaa tujifunze wimbo wa jumuiya ya Afrika mashariki, kwa kiswahili. Ya nini kiswahili hicho ? Wote katika watoto wa kiafrika walikuwa hawajui hata neno moja ya lugha zao za kuzaliwa. Na wote walikuwa ni watoto wa matajiri ambao, bila ya shaka, ni kile kizazi kipya ambacho Uganda inakitegemea ili kujenga mustakabali wenye mafanikio.

Na mafanikio siku hizi yanapatikana katika lugha za kimataifa tu. Sijui ni asimilia ngapi ya watoto hawa katika nchi ya Uganda ambao wamebahatika kuandikishiwa na wazazi wao katika shule kama hizo. Lakini ni kidogo. Nani katika nchi za Afrika mashariki ana uwezo wa kulipa dola 10 000 kila mwaka — na malipo hayo ni madogo kulingana na yale yanayotozwa, kwa mfano katika shule za kimarekani kama Kisu (HAPA) ambapo mtu hulipa si chini ya dola 20 000 kila mwaka. Wakati huo huo, watoto wa mikoa mingine, tuseme wa kaskazini karibu na mpaka wa Sudan, hawana hata madawati. Kwa mujibu au kwa msaada wa shule hizo, watoto wa vigogo watakabidhiwa kazi za baba, wakati watoto wa washamba watapewa jembe. Mtoto wa kigogo atarudi nyumbani baada ya kusoma Chuo kikuu Marekani kwa sababu nafasi wizarani inamsubiri. Si anaongea kimombo ? Kisha atakumbuka marafiki zake za shuleni, si wale wa Sweden, wa Japan, wa Brazil ? Kujenga uswahiba ni muhimu bwana ! Faida kwa nchi za Magharibi ni nyingi, hata kama mtoto huyo atakuja kuponda tabia mbaya ya wazungu (hapo tunakumbuka hadhira ya M7 kuhusu ndoa ya jinsia) kwa sababu mambo yake yote (na hapo tunasema "thank you International Schools"), vimeremeta, blingbling, kompyuta, gari na kadhalika zinapatikana Uzunguni. Licha ya vikorombwezo vile, pia ni dhana, risala, muono, zote za kumfanya kijana wa kigogo awe na starehe nyingi katika dunia hii ya utandawazi. Si amekunywa sharubati kupitia buruji za « international schools »? Awe mpinzani au mshabiki wa mambo ya Ughaibuni, hamna takilifu. Ngugi wa Thiong’o ama Mugabe ni sawa. Wote wana matanuzi.

                                 

Hapo hakuna haki wala usawa. Wakati watoto wa shule jina wanatakiwa wafyagie uwanja wa mpira kwa fagyo ya mjukuti (kwa kuwa « mwalimu hayupo »), watoto wa shule za kimataifa hupiga mbizi katika swimming pool. Faida kwa watoto waafrika wa shule hizo ni nyingi sana : kusoma katika mazingira ya fahari, kutumia lugha za kidunia, kuishi na watoto wengine matajiri ambao hutoka nchi mbalimbali, kualikwa na marafiki huko Ughaibuni wakati wa likizo, kusoma katika darasa lenye wanafunzi 15, kubahatika kusomeshwa na walimu wenye uelewa na umahiri mwingi, kuzoeleka na mazingira yenye mapambo, uzuri na nidhamu, na kadhalika. Wakati vishawishi hivi vyote vya fahari vinasaidia watoto wajenge tabia tiifu ya kusalimu amri zote za soko huria, shule za kienyeji zinachangia sana katika kuimarisha tabia tiifu ya kusalimu amri zote za siasa za ndani. Kwa kuwa shule hizo jina zenye vidarasa vitupu zinapuuzwa na viongozi wa « nchi hizo zisizotaka misaada », mtu asitegemee kupata kizazi kipya kitakachokuwa na sauti katika kupambana na maswala yaletayo udhulumu, ufisadi na ubedui. Penye udhaifu na uhaba wa elimu, uonevu na udhalimu hutawala. Lakini shule hizo jina zina ufanisi mkubwa sana. Kwanza inawafundisha watu kwamba lugha hizo za kienyeji ni kwa ajili ya nyumbani tu. Lakini asije mtu hapo kusema kwamba lugha zote hizo za nyumbani ni sawa na lugha za kidunia. Si kudharau lugha za kienyeji kusema kwamba ni lugha maskini. Ila umaskini wao unatakiwa. Tofauti na lugha zile za kidunia ambazo zina fahari za kweli kwa sababu ziliamka zamani sana, zikiwa zinatumiwa na watu ambao walitaka kuziendeleza kupitia asasi nyingi, mojawapo ni shule. Kijapani kuanzia karne 8, kifaransa kuanzia karne 11, kiengereza kuanzia karne 13, kiitaliano karne 14. Pili inawafundisha kwamba kila kitu ni utamaduni, hadi lugha. Achilia mbali hesabati, sayansi, falsafa, fasihi na kadhalika ambazo zina misingi katika nidhamu ya maarifa, urazini wa dhana, mantiki na ukweli wa fikra.

                         

Uwongo kadha umetawanyika. Umepamba moto. Kusema asiseme mtu kuwa lugha za kienyeji za Afrika zina maana. Wapi, wakati watoto wa vigogo hujiunga na shule za kimataifa ili nao pia wafikie hadhi na cheo kikubwa wakati watakapofikia umri mpevu. Nini maana yake kusema kwamba kiengereza ni lugha ya kitaifa (Kenya na Uganda) wakati ni wazi kwamba vijijini lugha hiyo ni lugha bubu tu ? Kuaridhia asiaridhie mtu kuwa mitaala hutungwa na wataalamu wa wizara ya elimu ya nchi husika wakati ni nchi ya kigeni, hasa Marekani, roho ya dunia, inayoongoza ngoma. Kuzingatia asizingatie mtu maadili ya kiafrika wakati shule hizo za kimataifa huziingiza maadili na desturi zilizosharabu mitindo na mikabala ya kikabila za nchi hizo za kigeni. Nasisitiza hapo, nimeandika kikabila. Nini maana ya kupinga kukeketwa kwa wasichana hapa na pale Afrika kupitia asasi za kimarekani wakati shule hizo za kimataifa zinaambukizia hoja zile tatanishi za kubadili jinsia ? Eti jinsia inaweza kubadilika baada ya muda.

                                             

Nashangaa kuona wananchi wengi wa Ufaransa wanavyopambana na serikali yao (inayoendesha shule kupitia wizara ya elimu) ili kuondoa kurejelea nadharia ya jinsia katika mitaala ya shule, mpaka wengi wanaamua kuandikisha watoto wao katika shule binafsi, wakati ambapo watoto wengi Waafrika wanasoma katika shule hizo. Kwa nini wazazi wa Afrika ambao huandikisha watoto hawa katika shule hizo hawaulizi ? Si wanalipa ? Isitoshe kwa nini shule hizo mara nyingi huacha kusomesha falsafa, fasihi na sayansi ambazo zilichangia sana kujenga mataifa yale ya nchi za Magharibi kupata matokeo ya fahari katika ubunifu ? Kwa nini shule hizo za kimataifa, kwa kifupi, zinafundisha masomo ya « uhondo » (entertainment) na burudani chungu nzima badala ya kusomesha masomo yale ambayo yalileta mafanikio makubwa katika historia ya nchi za kimagharibi ?


Inasikitisha kuona kwamba Afrika viongozi hawaachi kuzubaisha wananchi, lakini Ughaibuni yote mamoja. Halafu tutasikia hapa na pale kwamba nchi hizo zinatawaliwa, zinanyanyaswa kwa sababu ya ukoloni mambo leo. Na berere berere hizo zinasambazwa na wale wanaotetea lugha za kiafrika, lakini kwa kutumia kiengereza. Si watu wengi wanakubali kwanza kutawaliwa ? Na wanapenda kutawaliwa ? Si wanataka iwe hivyo ? Au wapinzani wapo ? Tusisahau kwamba binadamu ni mmoja. Kimaumbile ana matakwa na amekabidhiwa uwezekano wa jukumu na uhuru. Kusema kwamba mtu ametawaliwa na kuwa hana kauli ni kudharau binadamu na kumchukulia ni chombo tu. Ama pengine kwa sababu « misaada » na ufadhili huboronga maumbile ya binadamu, yaani matakwa yake, asije akawa na zihi na udole tena ? Hiyo ilikuwa ndiyo nadharia tete ya Immanuel Kant katika kitabu chake « Religion within the Limits of Reason Alone » (1793). Ikawa uzembe, utepetevu, uvivu, ajizi, kutojali, choyo, husuda… zimeshamiri mwishowe ukapatikana ubinafsi wa kiujamaa ? Balaa tu. Mzee Kaguta alisema lakini : « we don't need aid, it's not the solution but part of the problem for Africa ». Ndiyo bwana, lakini shule hizo za bizness bado zipo.

LA ZIADA :

Kuhusu ada za shule za kimataifa Tanzania : HAPA
Kiswahili na shule za kimataifa Kenya : HAPA


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni