19/09/2017

Urithi uliopotea Afrika (4) : tembo


Tanbihi : makala hizi zote katika mlolongo huu « urithi uliopotea Afrika » zimeandikwa mwaka 2017 ili zisomwe mwaka 2050. Maudhui yote yanaambatana na mazingira ya Afrika na wanyamapori wake. Inachukuliwa bayana kwamba viumbe wote hawa ambao wanagusiwa katika makala hizi wamepotea. Sababu zisizopingika zinafamahika wazi, nazo ni uharibifu wa mazingira pamoja na ongezeko hobela hobela la watu bara la Afrika.

---------------------------------------------

Tembo ama ndovu wa savana (Loxondota africana) pamoja na tembo wa msituni (Loxondota cyclotis) walikuwa wameenea kila sehemu ya Afrika. Shughuli za binadamu, pirika zake za kudharau uhai (kuzaa kwa wengi, kuzalisha na kuchuma kila kitu) na kutorithisha mapokeo ya wazee waliokufa zamani, ni katika shinikizo kubwa zilizoathiri vibaya spishi hii ya ajabu kiasi cha kuitokomeza katika mazingira yote ilikokuwa ikipatikana. Siku hizi tembo wachache wamebaki katika zoo za nchi za Magharibi na wachache wangali wanaishi kwa taabu katika vipori vilivyobaki Afrika ya kusini (Botswana na Namibia).

Kabla ya ukoloni wa kizungu, tembo walikuwa takriban milioni 20. Mwaka 1970, walipatikana milioni moja tu. Walizidi kupungua kwa kasi hadi kufikia tembo 496 000 mwaka 2007 na tembo 352 000 mwaka 2014. Kuanzia mwaka 2015, idadi ya tembo iliendelea kupungua kwa asilimia 8 kila mwaka. Juhudi zilizofanyika ili kuepuka maangamizi makubwa ya tembo hazikufua dafu. Hatua nyingi zilizotekelezwa na wanaharakati wengi wa hapa na pale pia zilishindikana. Asasi za serikali nyingi pamoja na zile zisizo za serikali ziliwania uokovu wa mnyama huyo lakini zote zilitelezwa kwa sababu ya kupuuza taathira moja tu, ile ya ongezeko la watu (kuhusu ongezeko la watu duniani HAPA). Wakati ule ule, asasi zile zilizojihusisha na ulinzi na hifadhi ya tembo zilikosa kupambana na swala hilo zito la mpango wa familia. Takriban zote (orodha za NGO hizo ziko chini ya ukurasa huu), pengine kwa sababu zilikuwa za kigeni, zilishindwa kwa kutokuwasilisha swala hilo kama ilivyotakikana, huku wakijitahidi kuhamasisha serikali ichukue hatua ya kudhibiti ongezeko la watu. Juu ya hayo, elimu ya nchi za Afrika mashariki ilizidi kusambaratika, huku kile kizazi kipya kikiendelea kupuuza hoja hiyo ya mazingira. Nani anajua maana halisi ya dhana ya mfumoikolojia ? Siku hizi watu wameongezeka wakiwa hawana hata nafasi ya kulima, wangali wako maskini, maji safi ni taabu na viumbe hai wote wamepotea. Hasara ni kubwa zaidi.


Tembo alikuwa ni mnyama aliyeishi kijamii, kwa vikundi vikundi. Kila kundi lilikuwa imara na tembo wote walikuwa wanahusiana kupitia mawasialano ya kiukoo. Tembo wa kike ambaye alikuwa ni mnyama wa miaka mingi katika kundi lake ndiye aliyekuwa anaongoza jamaa zake katika matembezi ya hapa na pale. Tembo wa kiume ambao walikuwa wamepita miaka kumi na mbili walikuwa huishi pamoja, katika kundi lao. Hivyo makundi makubwa yalikuwa ni makundi yenye tembo wengi wa kike pamoja na watoto wao. Makundi ya tembo wa kiume yalikuwa hayakupangwa vizuri ila yalikuwa ni aina ya mikusanyiko tu kwa kuwa yalikuwa si imara sana. Yaliondokewa mara kwa mara na baadhi ya tembo washirika kila mara dume alipofikwa na shauku. Hapo ndipo tembo huyo aliyekuwa na joto alipokwenda kuandamana na kundi lingine la kike lenye tembo wa kike aliyekuwa na joto pia. Kikubwa hapo ni kukumbuka kwamba makundi yote ya tembo yalikuwa yakifuatisha utaratibu fulani katika uhusiano. Tembo mkubwa na mzee zaidi katika kundi ndiye aliyekuwa kiongozi.

                                            

Tembo walikuwa si wanyama wenye makao maalumu. Walikuwa wanaranda porini kupitia njia walizozijua wenyewe kulingana na kupatikana kwa malisho ya miti pori. Matembezi yao pia yalikuwa yanategemea sana kupatikana kwa maji, nayo ni kigezo kikubwa kwao kwa kuwa kila tembo alikuwa ana haja ya maji kiasi cha lita 70 hadi 120 kila siku. Chakula chao kilikuwa cha kila aina, lakini cha kioto pekee, kama vile mizizi, mashina, magome na maganda ya miti, nyasi, majani, matunda, maua, mbegu, vikonyo na kadhalika, kutegemea na msimu. Tembo walikuwa na zana mahususi ili kujipatia chakula hicho. Walikuwa hutumia mkonga, meno ya pembe na miguu yao. Mfano tembo alikuwa na uwezo wa kuchimbua mzizi fulani kwa kutumia mguu wake, kisha aliung’oa kwa mkonga au meno yake ili hatimaye aubebe kwa mkonga hadi kinywa chake. Nao mzizi ukiwa na udongo ataukung’uta barabara kabla ya kuutafuna. Alikuwa na uwezo pia wa kujivuta juu huku akisimama juu ya miguu yake ya nyuma ili kufikia matawi au matunda fulani yaliyokuwa kileleni kwa mti. Na juhudi hizo ziliposhindikana, alikuwa hasiti kuuangusha mti mzima ili familia yake pia hujifaidi nao. Mkonga wake ulikuwa ni zana nzuri iliyokuwa na matumizi mengi, ikiwa ni pamoja na kuvuta maji na kuyapeleka katika kinywa. Kwa kuwa mkonga huo ulikuwa na umbo wa bomba, ulikuwa unateka kiasi cha lita nne kila ulipochota maji. Tembo wengi walionusurika kutoka katika mtego wa chuma walikuwa hukatwa kipande cha mkonga. Endapo mkonga ulikuwa umepooza kiasi hicho, ilikuwa vigumu kwa vilema hawa kuishi muda mrefu kwa kukosa kifaa hicho cha kuwasaidia kula na kunywa.
 
                                          

Pembe zake pia zilimsaidia kupata chakula kwa mfano kubandua magome ya miti na kuvunja matawi na kupasua vigogo. Mbali na kuwa kifaa cha kujipatia chakula, pembe hizo zilitumika pia kama silaha katika mapambano yaliyotokezea mara kwa mara baina ya tembo dume. Lakini mapigano hayo yalikuwa nadra. Kwa jumla, tembo alikuwa ni mnyama mpole na mtulivu sana ambaye hushinda kutwa kula. Ndio maana alikuwa hatembei sana (kilometa 6 hadi 10) kila siku, ikiwa chakula ni cha kutosha katika eneo lake, hususan wakati wa msimu wa mvua. Msimu wa kiangazi ndio uliompeleka mbali, hususan vijito na madimbwi ya maji zikikaukiana. Ndipo tembo walipoonekana huku wakijitokezea katika maeneo ya watu wakiharibu vibaya mashamba na mavuno yao. Mbinu zile za kuwazuia wasiingie humo zilikuwepo, kwa mfano kuchimba handaki ama kuweka mizinga ya nyuki kwenye mizunguko ya mbuga zile walimoishi. Lakini uzembe na pengine ukatili wa binadamu ndio uliosababisha mauaji ya tembo wengi. Kuhifadhi ni kazi kubwa kushinda kuua.
  

Tembo walikuwa hutoa na husikia sauti ya chini sana na hata baadhi ya sauti nyingine ambazo binadamu hazipati. Wana sayansi walithibitisha kwamba walikuwa wana sauti kubwa ya aina nne ambazo kila moja ilikuwa na utepe wa marudio mwingi kulingana na mzio, mwendo na kipindi cha mlio mwenyewe. Hivyo tembo alikuwa ni mnyama aliyekuwa hutumia utepe mkuwa sana wa sauti zile zilizomsaidia kuwasilisha ujumbe fulani, hususan hisia na ghamu zake. Kikubwa hapo ni kukumbuka kwamba kila tembo alikuwa ana sauti yake ya kibinafsi ambayo ilimtofautisha na wengine katika kundi lake. Sauti hizo chukuzi zifuatazo zilikuwa zinabeba ishara ya kila aina, kitu ambacho kilidhibitisha kwamba tembo alikuwa ni mnyama mwenye ishara zake za kipekee :
  • Tembo alikuwa hujua kuvuma kwa kutumia sauti ya chini ambayo binadamu haisikii. Huo uvumi ulikuwa hutumika wakati tembo walitaka kuwasiliana na tembo wengine wa mbali. Sauti hiyo ya msondo ilitozwa kupitia 14 Hz na 103 dB na ilikuwa ina nguvu ya kutembea kiasi cha kilometa kadha. Ilitumika hasa kati ya makundi mbalimbali, kati ya makundi ya tembo wa jinsia tofauti. 
  • Alikuwa pia hungurumisha sauti iliyosikika karibu, hasa katika kundi lenyewe. Ngurumo hizo zilikuwa na maana fulani, hasa katika maamkizi ama kuwasilisha hofu au maumivu fulani. Wakati mwingine sauti hiyo ilipaa ili kusudi kutisha wanyama wengine wakali kama simba au faru.
  • Pia alikuwa anapiga tarumbeta, sauti ya kuonyesha ghadhabu. Sauti hiyo ilikuwa ina namnisho (modulation) nyingi, kupitia vingoto vidogo hadi vitutumo fulani, ya kuwasilisha hisia mbalimbali zenye hofu, nyingine zenye uchangamfu, kutegemea na muktadha ule uliowakumba.
  • Vilikuwa pia vilio vingi vya kuwasilisha ishara nyingine kama vile vilalamiko fulani vya kuomba msaada, kama walivyofanya tembo wachanga.
Wana sayansi waligundua pia, katika tafiti zilivyofanyika kuanzia mwaka 2010 na mbele, kwamba tembo walikuwa hutumia pia vishindo vilivyosafiri ardhini ambavyo mawimbi yake yalitozwa kupitia miguu. Vishindo vile vilikuwa vina nguvu ya kusafiri masafa marefu, kiasi kilometa kadha (soma HAPA, kwa kiengereza).

                                          

Katika mfumo huo wa mawasiliano, mbali na matumizi ya sauti kadha, tembo walikuwa ni wanyama werevu sana katika matumizi ya ishara nyingine kama vile za miguso ama za harufu. Kila ishara, kwa mfano kuinua au kuzungusha mkunga kwa namna fulani, ilikuwa ina maana fulani. Masikio yake pia, kama yakipepea ama yakitandazwa, yalikuwa yanabeba kusudio fulani. Kikao chake pia, akiwa amekaa chonjo, ama akiwa ametuwama pasi na kusogea mbele, ama akiwa ameinua kichwa chake juu, na jinsi nyingine nyingi zilikuwa zina ishara zenye maana (soma HAPA, kwa kiengereza).


Tembo walipotea kabisa Afrika kwa sababu nyingi. Alikuwa ni spishi dhaifu kwa sababu kipindi cha kubeba mimba kilikuwa kirefu, kiasi miezi 22. Isitoshe, mimba ya kwanza kwa tembo jike ilikuwa haipatikani kabla ya kutimia miaka 10 au 11. Kisha, tunajua kwamba kulikuwepo kipindi cha miaka 4 hadi 9 baina ya mimba mbili, kutegemea na hali ya mazingira na muundo wa kundi la tembo. Vigezo hivyo vilikuwa vimemponza kiasi fulani kwa kutomwezesha atunge mimba nyingi kisha spishi iweze kujihifadhi vizuri. La kuihatarisha zaidi spishi hiyo lilikuwa mimba yenyewe ambayo ilikuwa ni ya mtoto mmoja. Kupotea kwa mnyama huyo wa ajabu ni balaa kubwa sana kwa binadamu. Ni aibu na hizaya kubwa mno. Pamoja na kwamba alikuwa huwa ni mnyama haribifu, pia ni mnyama ambaye huimarisha misingi ya uhai. Tembo akipotea, ni spishi nyingi mno ambazo zilipotea pia, mchakato ambao pia ulileta maafa makubwa katika maisha ya usoni ya binadamu. Usasa, umimi, unafsi (selfishness), sifa mbaya hizo ndizo ambazo zimechipuka katika ujinga na uzembe zikamwainisha binadamu katika spishi zote mharabu. Kwa mujibu wa maendeleo endelevu, leo hii, mwaka 2050, tumefika kwenye umasikini endelevu.Tovuti muhimu kuhusu tabia, mienendo, maumbile, hisia, mawasiliano za tembo :

Elephant voices : HAPA

Tovuti nyingine kadha:

TEPS Tanzania : HAPA
Tembo wa Selous : HAPA
Okoa tembo wa Tanzania : HAPA
Tsavo Trust Kenya : HAPA
Amboseli Kenya : HAPA
African Parks : HAPA
Big Life : HAPA

Kuhusu kupotea kwa uhai katika dunia : HAPA

Kuhusu kuangamizwa kwa ndovu wa Tanzania : HAPAHakuna maoni:

Chapisha Maoni