17/10/2017

Yambo Ouologuem amefariki


Yambo Ouologuem (1940-2017) amefariki, tarehe 14 ya mwezi huo wa oktoba. Hapa Afrika Mashariki tunakopenda itikadi za umoja wa Afrika kuliko fasihi, Ouologuem ni mgeni kabisa. Hatujui jina lake, hatujui vitabu vyake. Lakini ni mwafrika aliyezaliwa Mali. Anajulikana sana katika dunia ya fasihi, isiyokuwa na itikadi ya umoja. Tatizo ni kwamba Waafrika wenzake walimchukia kwa sababu alikuwa msanii mkweli. Na ukweli unauma. Alikuwa hapendi maoni yenye busara ya kawaida, yale yaliyoshamiri katika jamii zile zinazopendelea utaratibu wa mwafaka kuliko ukinzani. Ndiyo asili ya chuki na bughudha alizolimbikiziwa. Afrika msanii asiwe na unafsi mwingi bali afuate mkondo, asijitenge na jamaa zake bali awe msikivu na mnyofu, asiandike katika lugha chafu iliyokithiri katika jamii yake bali aitakase takase kama tunavyotahiri mwari jandoni. Awe mtiifu mwenye insafu kupindukia. Lakini Ouologuem naye alikuwa ni mwasi na mpinduzi. Hivyo alikuwa si walii wala mtakatifu. Wengi walimwotea kashfa.

Wasanii wengine wamepata umaarufu baada ya kufungwa jela, huyo Ouologuem alipata umaarufu baada ya kuandika vitabu vyake. Hapo kuna siasa na huku kuna usanii. Lakini umaarufu ule ulimchongea. Pengine kwa sababu ya uchoyo na husuda zilivyopamba moto katika jamii za Afrika. Mbinu za kumwangusha mtu mwenye umahiri mwingi hazikosekani. Wacha uchawi ule uliozoeleka mote, sitaji watoto wale wa Nigeria wanaoangamizwa kwa tuhuma ya urogo wala mazeruzeru wa Tanzania wanaoishi katika hofu ya kupungukiwa na viungo vyao, kwa kuwa umbea na uchimvi umeondokea ni mbinu za kisasa ambazo zimebarikiwa katika muktadha mpya wa mawasiliano ya kileo. Naye Ouologuem kapigwa dunga. Filihali kuandika kitabu chake cha kwanza, sifa ya Ouologuem ikachafuka na kazi yake kupondwa. Mtungaji akatukanwa na kukosa radhi ya wenzake. Na wenzake katika dunia ya usanii si raia na jamaa zake tu. Dunia nzima.

Huko Ufaransa kwanza alikopata kuchapishwa kitabu chake cha kwanza, Le devoir de violence (Bound to Violence), mwaka 1968, baada ya kupata tuzo adhimu ya fasihi iitwayo Prix Renaudot, Ouologuem alirushiwa kashfa ya kughushi baadhi ya maandiko yake na kutozingatia hakimiliki za usanii. Na kweli vidondoo au matini kadha ya kitabu chake zimetoka katika vitabu vingine maarufu kama vile vya Rimbaud, Maupassant na Graham Greene. Na tuhuma hizo za kudai kwamba vipande vya kitabu hicho vimenukuliwa moja kwa moja kutoka katika vitabu vingine pasipo kukiri kunukuu huko zilimwathiri sana Ouologuem hadi kuamua kutoandika tena. Lakini athari hizo mbaya zilileta athari nzuri pia kwa kuwa shutuma hizi za wizi wa kisanii zilizusha mjadala mzuri kuhusu jinsi ambavyo msanii yeyote hutegemea jasho la wengine. Ghushi na utohozi ni dhana ambazo ziko karibu sana. Hilo tunalijua leo.

                                

Lakini mwaka 1968 ulikuwa ni kipindi cha itikadi nyingine sahilishi. Tena itikadi chakavu lakini gundi. Kwa kifupi, Mzungu ni mbaya na Mwafrika ni mzuri. Yambo Ouologuem, ambaye alikuwa hana itikadi hizo, kwa kuwa hajali kabisa udaku na maneno ya gengeni, vile vile hana mshipa ule wa kuchukulia Afrika kuwa chanzo cha mawazo mengi ya kifalsafa. Dhana ile ya Negritude (falsafa ya Ugolo) haikumpiga mshipa. Yeye haoni sababu ya kutofautisha Mzungu na Mwafrika. Hapo ndipo balaa ilipomkumba. Si kupambana tu na usanii na ufalsafa wa Senghor ambao, kimaudhui, ulitilia mkazo historia nzuri za Afrika kabla ya ukoloni wa kizungu, pia ni kukabili ujinga uliozagaa Afrika tangu na tangu. Kwa kifupi, maoni shamirishi ya enzi ile ilikuwa inachukulia bayana kwamba kabla ya ukoloni wa kizungu, mambo yalikuwa shwari kabisa. Yambo Ouologuem naye alitunga kitabu hicho akisisitiza, kinyume na kilichotakikana wakati huo, kwamba kabla ya ukoloni, mambo yalikuwa mabaya pia. Ndipo Senghor alipojivuta pale akasema : « Msanii hushindwa kuandika kitabu chenye maana ikiwa anaponda enzi ya wazee waliokufa zamani ». Hukumu ilikatwa. Mwafaka ukarudi ukatawala tena.

Ukweli ni kwamba Bound to Violence ni kitabu kilichojaa mada pinduzi na kauli mgongano ambazo, hususan siku hizi Afrika mashariki, hazijagusa akili ya wasanii wengi wa kiafrika kwa sababu ya kutokubalika. Kwa kuwa ni kitabu cha kubuni, kilijaa tasnifa na shani fumbifu. Jambo ambalo tunalisahau wakati tunazingatia uhalisia tu. Msanii wa fasihi si kazi yake kuhubiri. Wala kuhamasisha watu na kuwasilisha ujumbe fulani. Kazi yake kubuni tu. Fasihi bora ni ile inayotutoa katika uzoefu fulani. Inatufanya tuangazie dunia kupitia macho mapya. Ni kama kuzaliwa upya. Hadi tugundue kwamba maoni yetu yalikuwa hayana misingi. Nadhani kwamba Le devoir de violence imekamilika kwa kutimiza dhima hiyo. Lakini katika dunia ambayo inazidi kujikunyata kwa kutokuwa na utamaduni wa fasihi, udikteta na uhayawani utazidi kukithiri. Kujikosoa bado.

Fasihi ni tishio kwa dikteta. Na udikteta wa siku hizi una ujanja mwingi mno hadi kuwa na uwezo wa kughushi fasihi bushoke, ama fasihi bandia ambayo inajidai kuyaelimishia jamii maadili na mapendekezo mazuri. Vitabu vya Ouologuem ni kinyume cha mkabala huo. Yeye mwenyewe alikataa kuzifanyia kazi serikali za Ufaransa na Mali. Aliwahi kufundisha katika shule za serikali lakini akapendelea kujiuzulu na kurudi kwao. Bila ya shaka, marupurupu, posho na vitegemeo vingine vya serikali zilimkirihisha kwa sababu ni katika vipengele mbalimbali ambavyo vinaua ilhamu ya msanii, vinampotosha vibaya. Maisha ya marehemu Ouologuem yanafikirisha na yanasailisha : nini maana ya usanii usiokuwa huria ? Husemekana kuwa kazi ya usanii ni kutuliza jamii, kuiliwaza wakati vurugu na ghasia zinapotokezea. Kuimarisha uzalendo na kuendeleza hisia za utaifa. Wengi katika wasanii maarufu duniani waliitilia shaka dhima hizo huku wakizishuku vibaya. Voltaire, Hugo, Orwel, Huxley, Celine na wengine wengi kama Sony Labou Tansi wa Kongo (HAPA), Ahmadou Kourouma kutoka Kodivaa (HAPA) na Yambo Ouologuem wa Mali (HAPA) walitumia kipaji chao ili kuwasilisha ubishi na upinzani katika jamii. Naye marehemu ameshalipiwa fidia. Kote kunako uhuru ameshapata kutafsiriwa, si chini ya lugha kumi. Kiswahili je ? Thubutu !


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni