30/11/2017

Karakana ya msanii


Kuna fasihi na kuna dunia. Msanii kazi yake ni kufasili dunia. Na katika kazi hiyo, ikiwa anatumia muono wake, basi atakuwa ni mtunzi na mgunduzi. Kipaji chake kinategemea ilhamu na hisia. Swala linakuja hapo : endapo dunia imeshafasiliwa kupitia ndimi nyingi mbali mbali, ama kupitia uchanganuzi kupindukia, kwa sababu binadamu ni maumbile yake kumaanisha kinachomkumba — mathalan asasi nyingi zinachangia, kila wakati, kutuambia jinsi dunia ilivyo — ama kupitia lugha ambayo ni duni kabisa, je msanii atakuwa na uwezo wa kutunga kitu ambacho kitakuwa kimejaa ubunifu ?

Kwa kifupi, ikiwa lugha imebaki katika hali ya kubambanya bambanya dunia, huku ikiwa imejaa maoni gundi (cliché), ama ikiwa imesharabu kauli chakavu, kwa jumla maoni potovu, je msanii atakuwa na uwezo wa kuinua lugha hiyo mbovu hadi kuifinyanga kisanii ? Maoni gundi na lugha ya mwafaka — kwa mfano, maneno yale yale yanayoambukiza lugha bunifu kutoka jamii ambayo yanatumika kila wakati — si vikwazo tu, ni balaa kwa kuwa ndiyo inayomlazimisha msanii apambane nayo kwanza ili baadaye apate kusawiri lugha yenye shani. Kazi kubwa. Na ikishindikana, basi atakuwa si msanii.

                                                      

Katika nchi nyingi, njia zote za ubunifu zimefungwa. Afrika mashariki zimefungwa kwa sababu mbalimbali. Kwanza elimu ni finyu kabisa. Pili, shule zote ni shule jina (HAPA). Tatu kisiasa, asasi zile za serikali pamoja na vyombo vya habari zinasalimu amri za wakubwa ili ipatikane hali ya mwafaka. Msanii ataambiwa ni msanii bora akiwa ameandika kitabu kitakachosomwa shuleni, ama ikiwa anawasilisha jumbe ambazo jamii pekee imepewa haki ya kuzihalalisha. Waandishi wa habari, baadhi ya wanazuoni na vile vitoa vitabu vichache — ambao wanabamba milango yote ya uchapishaji — ndio masetla wa siku hizi. Ndio wanaotoa katekisimu ama sura halali — vielekezo na maadili — ili wewe msanii ujue kunyenyekea na kutii. Na usiwe na unafsi. Kuwa na upekee ni kuvunja kanuni na viongozo vile. Ni haramu.

Matokeo yake ni kwamba dunia haieleweki. Na vitabu vingi vya fasihi havisaidii kuielewa kwa kuwa hutumia lugha mwafaka. Hivyo fasihi imechafuka kwa kupambwa na habari nyingi, habari ambazo hazina miguu wala vichwa. Taarifa za chambilecho, stori zile za tovuti za gengeni, visa na mikasa za mitaani, kiswahili hicho cha vizito (« bwana tumefikwa na changamoto kubwa ! »), umbea na udaku wa masupa staa. Uchoshi wa vikorombwezo na vichezeshi vile vya kisasa. Lugha iliyochoka taaban. Matukio yote yako mitaani, penye skani za kina mshkaji, katika magazeti ya mapaparazi, kwa kifupi katika « utamaduni » wa watu. Busara ya maoni. Eti hizo ndizo habari zinazostahili kubebwa katika fasihi. Kwa sababu tumeshazisikia, zinavuma kote, kutoka maskani hadi Ikulu, tunazipenda mno. Wee msanii utuletee visa hivyo ! Si unajua kuandika ? Kisha utuelimishe bwana ! Ngoja shemeji yangu anajua mchapishaji yule… kamwendee basi, hakuna resi huko !

Kwa bahati nzuri, fasihi si plasta. Wala si burudani kwa maana ya burudani ya kina bwege kamtozeni. Na fasihi si msaafu. Hakuna fasihi inayo uwezo wa kuhamasisha na kuelimisha jamii, si kweli. Fasihi bora ndiyo ile inayoshtua msomaji, kwa kuyapindulia mbali maoni yake chakavu, na wakati mwingine kumchukia, asije akawa tena mtu mtiifu — au raia mwema katika mazingira ya mwafaka, msomaji wa paukwa pakawa — asije akawa mpiga kura wa mgombea mmoja.  Fasihi si kuwasilisha ujumbe, si kumaanisha yanayokubalika kote, si kudhamiria amani na ukombozi fulani, si kuimarisha mfumo ulioshikamana, si kuungama wala kukiri. Yote hayo ni uwongo wa wanazuoni ambao wanataka kumnyamazisha mwana fasihi asiwe mtu huru akiwaandikia wasomaji huru.

Huko juu, katika darasa la chuo kikuu (kwenye kitivo cha kudhibiti jamii ?), Profesa anauliza : huyo msanii alitumia tafsida ngapi ? sitiari na tashihisi ngapi ? Nawe mwanafunzi umefurahi kwa sababu umepata maksi nyingi. Kwani kupima fasihi ni kuhesabu ? Na kweli, unajua kusoma. Hongera, lakini unaweza ? Kinyume na hayo, akiingia katika karakana ya msanii, mtu atashangaa kuona kwamba hakuna vifaa, hakuna mbinu, hakuna farasi ya kupasua na kuranda maneno. Atakuta vita tu, ngondo, vurumai. Wasiwasi. Msanii hapigi ngumi, lakini anapigana na wakati wake ili kukiuka na kupindua maana zilizomfikia. Usanii si mchezo. Ni shinikizo kubwa, chagizo ya kuchosha. Atafanyaje msanii ili kufumua kitu ambacho kimeshafumwa, kusiriba udongo uliokwisha kukauka, kutomea kuta ambazo zimeshapigwa plasta ? Si inabidi kubomoa kwanza, ili kujenga upya ? Kubuni tu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni