23/11/2017

Kuuliza si ujinga ? Afrika na sayansi...


Baadhi ya wanyamapori wamepata kuonekana kwenye tovuti mbalimbali kwa sababu ya sifa za ajabu. Kwa mfano duma ndiye mmojawapo anayejulikana kwa sababu ana mbio wa kasi mno kushinda wanyama wote — kitu ambacho si kweli kwa sababu baadhi ya ndege wanaruka kwa kufikia upesi mwingi kushinda duma — au tembo kwa kuwa ni mnyama mkubwa zaidi anayeishi nchi kavu. Twiga naye pia anapendeza kwa sababu ana shingo ndefu. Sifa hizo zote za kustaajabisha mtu ambazo zinatajika mara kwa mara kwenye tovuti kadha zinaonyesha jinsi binadamu anavyokuwa mjinga wakati anapogeukia maumbile na uhai unaomzunguka. Binadamu kazi yake ni kujiangazia tu. Kujikwatua, kujitazama na kujidai ana makuu. Na bila shaka, kadiri wanyamapori hawa walivyozidi kupotea kabisa ndivyo sisi binadamu tulivyofikwa na majivuno. Mbali na kupotea kwa viumbe vyote, sisi tumepoteza pia utepe au kipimio cha kujipimia kitabia.

Twiga si mnyama wa ajabu kwa sababu ni mrefu. Ni mnyama wa ajabu kwa sababu urefu wa shingo yake ni aina ya changamoto kibayolojia. Nakumbuka siku moja nilipokuwa nimefikwa na watoto wa shule huku nikiwa natumia darumbili ili kuangazia twiga waliokuwa wakitembea katika mbuga wa Masai Mara. Nikazumgumza nao nikawaelezea twiga alivyo. Nikawaambia jinsi twiga alivyoumbwa, urefu wake, miondoko yake isiyokuwa ya kawaida, tabia yake ya kula na kunywa na kadhalika. Mambo mengi ya kutuonyesha kwamba sisi wanadamu tuna maringo mengi. Hatuvipimi viumbe vile kama twiga kwa sababu hatutaki kujipima sisi. Pamoja na kwamba ni jambo la kumsaidia twiga ajiepuke na balaa fulani — kuwakimbia wanyama wengine wakali — shingo yake na urefu wake kwa jumla pia ni udhaifu mkubwa. Kwa sababu tunajua kwamba ubongo wa viumbe wote unahitaji damu. Sasa, je mnafiriri huyo mnyama atapataje damu itembezwe hadi ubongo wake ? Halafu damu ikishafika katika ubongo wa twiga huyo, je kushuka kwake si kunaweza kumwathiri vibaya ? Na tunajua kuwa maji ya tangi yakishuka katika mabomba yetu nyumbani mwetu yanapata presha nyingi. Hivyo basi, damu ile si itashuka kwa nguvu pia kutoka juu kiasi cha kumwathiri huyo mnyama ? Hivyo, huyo mnyama huishi vipi ?Haya maswala yote ni maswala ya kisayansi. Nilipokuja kuongea na mwalimu wa watoto wale, ndiyo mada tuliyogusia kidogo. Tukaungama kwamba sayansi si taaluma ambayo hufundishwa vizuri Kenya, seuze katika nchi nyingi za Afrika, ambapo hajatokezea mwana sayansi aliyenyakua tuzo ya Nobel. Sayansi ni taaluma inayosaili kisichoonekana. Maoni (kwa maana ya opinion) ni kauli ambayo haijatoboa kiwambo kile cha imani ambayo inakubaliwa na watu wengi. Kuona si kudhani. Kuona ni kuamini tunachoona. Mfano, twiga ni mnyama mrefu (kuona) wakati urefu wa kitu au kiumbe si hoja, kwa sababu inategemea yule anaangazia urefu ule. Paka ni mrefu sana akilinganishwa na panya. Hoja yenye maana ya kisayansi ni hivi : urefu wa mnyama huyo unawezekanaje wakati maumbile ya mamalia wote hayaruhusu ubongo usiwe mbali sana na moyo (kudhani) ? Ndipo udadisi wa mwana sayansi, ukiwa umechochewa kiasi cha kumpeleka katika hali ya kutunga nadharia tete (hypotheses) mpya, ndipo utamsaidia kutoka katika hadaa ya kuona akakubali kuingia katika uyakini wa kudhani. Na kadhalika, hadi tunagundua kwamba damu hutembea kwa msaada wa moyo mkubwa na valvu mahususi ambazo twiga ameumbiwa nazo katika shingo yake. Nduni hizo zote ni za kipekee kwa sababu zinamsaidia mnyama huyo kuishi bila matatizo.


               

Ukosefu wa udadisi ni balaa kubwa. Ni mwanzo wa ujinga. Mtoto, kufuatana na tabia yake, huuliza kila wakati. Anapenda kuuliza “kwa nini”. Na sisi wazazi wake na watu wazima tunajidai kwamba sisi ndio tunaojua kila kitu. Kwa nini twiga ana shingo ndefu, kwa nini punda milia ana mistari, kwa nini simba dume ana ushungi mkubwa, kwa nini, kwa nini, kwa nini. Sisi watu wazima husema “ah upuuzi mtupu !”.     

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni