14/11/2017

Urithi uliopotea Afrika (5) : mandhari


Tanbihi : makala hizi zote katika mlolongo huu « urithi uliopotea Afrika » zimeandikwa mwaka 2017 ili zisomwe mwaka 2050. Maudhui yote yanaambatana na mazingira ya Afrika na wanyamapori wake. Inachukuliwa bayana kwamba viumbe wote hawa ambao wanagusiwa katika makala hizi wamepotea. Sababu zisizopingika zinafamahika wazi, nazo ni uharibifu wa mazingira pamoja na ongezeko hobela hobela la watu bara la Afrika.


-------------------------------------

Sisi tuliowahi kuishi karne 20 na mwanzo wa karne 21, tulibahatika kujaaliwa dunia safi iliyotuletea thawabu kupindukia. Poleni sana nyinyi vijana mnaoishi mwaka huo 2050. Sisi tuliofariki tunashukuru Mungu. Tulipata kuishi katika mazingira mazuri, yenye viumbe wa kila aina, ndege kwa mamalia, samaki kwa repitilia, wadudu kwa vidubini. Mnajua binadamu alivyo. Tamaa, utashi, ulafi, uroho, kiburi, ujeuri, heshima jina, adabu hewa, shauku, majikwezo, ari, eti utamaduni. Kwa hivyo, viumbe wote, fyon ! Tumefyeka. Tumetega. Tumeuza. Tumekula. Mpaka tumekinai. Tumeshiba. Amdulila. Nakumbuka nilipokwenda Nakuru katika miaka ya themanini. Kenya huko. Bado ulikuwa ni mji mdogo, penye utulivu kwa sababu ya wakazi wachache. Siku hizi — na majuzi niliupitia — utajisikia umefika kwenye viunga vichafu vya Nairobi au Lagos, vibanda vya kujiinamia mbavu za mbwa, majengo ya udongo poromoka, mitaa ya Mchafu koge na maskani za Unajisi Furi. Kelele, honi, ingia toka, simile simile, ghasia, uchafu, pirika za kila aina, yaani mtindo wa binadamu. Mambo kuvunda tu. Si la kustaajabisha. Waandishi bora wameshasema :

« Wingi, wingi, wingi. Chukua, chukua, chukua. Kusanya, kusanya, kusanya. Pika, pika, pika. Pakua, pakua, pakua. Tumia, tumia, tumia. Kila mtu anataka kuvuka mpaka wa kupata ingawa wengi hawapati hata kidogo. Mazingira yanaharibiwa. Anga, pwani, mito, maziwa, ardhi. Kote kuna hujuma. Kote kuna wimbi kubwa la matumizi na fujo ! » (Said Mohamed, Mkamandume, uk. 289)

Zamani bara la Afrika lilikuwa lina hazina kubwa. Lilikuwa ni kama safina, yaani kimbilio kwa kila kiumbe. Siku hizi pakavu. Unyamavu wa kaburi. Ngurumbili na makoranyoka chungu nzima. Kila kona, hadi kileleni kwa milima. Zahama tu. Kulikuwa na mapori mazuri, miti ya ajabu, misitu ya kupendeza, mito na chemchemi safi. Maji angavu, yaliyoonyesha. Hewa si kitu adimu. Mwangaza mbichi. Kote kulitumbuizwa kwa vifijo na visauti vya baragu, chozi na virumbizi. Dunia ilikuwa kama katika nchi ya Busutamu alikohamia Utubora. Vipepeo vizuri vilikuwa haviishi katika dunia ya kufikirika. Uhai ulikuwa bado si kitu cha kuenzi. Kulikuwa na hifadhi, zile za mbuga na nyika kubwa sana, kwa kuwa tulikuwa tunafikiri kwamba wanyamapori walikuwa na maagizo ya kutuachia. Haki zao ni zetu. Lakini sisi hatukuzingatia. Upuuzi wetu ukazidi na badala ya kuerevuka tukazidi kuzinza kichwa na kujishaua.  

                                       

Mimi si mwafrika. Sina ngozi nyeusi. Sina nywele za kipilipili. Zangu za singa. Tunatofautiana. Haya. Kumbe wewe na mimi tunapiga ngoma ile ile. Ingawa kila mmoja huvutia ngozi kwake. Si tunawambana ? Wewe na mimi, tumeshawahi kutupa sumu za kemikali majini — si vibwakuzi vile tunavyotumia nyumbani mwetu ? Tumesharusha moshi chafu hewani, tumeshaendesha gari aina ya shangingi, tumefuja migodi ya kuchafulia mazingira ya vijukuu wetu, tumekula chakula kitokacho ng’ambu huko Ughaibuni au Japan, tumesafiri kila pembe za dunia, na hata viraba vyako vilikuwa vinametameta wakati ulipokuwa mdogo, tumepiga maji makali — wacha machozi ya simba na supu ya mawe — tukawa chicha ya kufa mtu, tumewasha taa usiku wa manane, tumekubali kuleta maji katika jangwa, sikwambii theluji ile ya Kilimanjaro. Si tuliwahi kuiyeyusha ? Kwa nguvu zetu. Na akili zetu. Si Wazungu walifanikiwa kuyeyusha barafu ya Akitia, na kuzuia Gulf Stream, na kufukia takataka zile za urani katika ardhi, chini kwa chini ? Binadamu ana nguvu, jamaani ! Hivyo tumefurahia maisha, tumeenjoy sana kwa burudani hizo tele.

Tumefaidi yaani. Tumekula sana. Mpaka kujichana. Na vituko vilikuwa vingi. Michapo na mizaha chungu nzima. Raha tu. Starehe za kujirusha kutwa kucha. Raha ya maovu.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni