10/01/2018

Husuda na uchoyo katika kuhifadhi mazingira : mfano wa Queen Elizabeth ya Uganda


Walipoondoka Afrika, wakoloni wa kizungu waliacha miundombinu mingi. Si mitandao ya barabara na ya reli tu (ambayo siku hizi imeharibika), bali waliacha pia hifadhi na mbuga za wanyamapori ambazo walizichukulia ni aina ya urithi mkubwa wa Afrika pamoja na wa dunia. Wakoloni hawakuelewa kwamba Afrika watu wana « utamaduni » wao au, kwa maneno mengine, falsafa na muono wa kienyeji. Katika muktadha wa Afrika, falsafa hiyo inazingatia sera ya « raha ya maovu », kama nilivyoiita miaka michache nyuma, nikautumia usemi huo kwa ajili ya anwani ya riwaya yangu ya kwanza, nayo inakazia furaha anajipatia mtu anapojikuta ameshinda kutesa mwenzake hadi kumtia udhia na uharibifu fulani. Kwa mfano, kuona kwamba jirani yangu ameanguka katika mpango wa kuezeka nyumba yake kwa mabati ni jambo linalonifurahisha kupita kiasi. Sababu zake ni wazi, nazo hazikutiliwa maanani na wakoloni, ni uchoyo, husuda na hiana. Kusikia raha ya maovu, ni kuharakisha kubomoa kwanza ili nisije nikabomolewe na wengine. Afrika hii ya mashariki mtu hupendelea kuangamiza kuliko kujenga na kubuni. Hupendelea kuchafua kuliko kusafisha. Katika riwaya yangu niliwahi kufinyanga mhusika ambayo jina lake ni Kadhi ambaye, mwisho wa riwaya, hutoa maelezo kuhusu « utamaduni » huo. Anasema :

« Ubaya una shukurani. Mtu akifanya ubaya, basi roho yake inafurahi, kwa sababu aliyetaka kumtesa mwenzake, basi ameshateseka, sasa anapita kucheka : ‘eh eh ! Kazi yangu ile !’ Anajifurahisha anajikuta yeye yuko katika raha mustajaba. Wengineo wakimchukia yule, kwa sababu ameshafanya ubaya basi wanakongamana wanaarikana kucheka na kufurahi, wanathubutu kuchinja mbuzi, kuku kutokana na yule alivyopatikana, kwa sababu alikuwa anawatia udhia, labda alikuwa anawambia maneno ya haki au ya sheria, basi wale wanachukia, kwa sababu ukweli unauma katika dunia, si mwarabu, si mhindi, si mzungu, si mswahili… »

Basi « utamaduni » huo mkubwa una nguvu nyingi. Nguvu ya kuteketeza kila kitu. Huenda binadamu hajapata nguvu nyingi kama hiyo. Na mgeni akiangazia jinsi mambo yanavyozidi kusambaratika hapa na pale katika nchi hizo, bila shaka atajitahidi kusogeza uchambuzi mwingi huku akisema kuwa vikwazo fulani katika jamii viko vingi, sijui watu hawajaelimishwa, ni maskini wa kutupwa, sijui siasa mbaya, rushwa na ufisadi zimekithiri, na kadhalika. Mwanazuoni wa kienyeji naye, bila shaka, atasema hizo zote ni athari za kasumba au siasa ya baada-ya-ukoloni. Kila mtu na duka lake. Lakini kigezo kikubwa kile cha uchoyo au husuda, bado. Ukweli ni kwamba husuda na uchoyo ni hisia ambazo hutokeza katika matabaka yote ya jamii. Waandishi maarufu duniani wameshaelezea jinsi ambavyo zimepamba moto hadi katika ngazi ya juu katika jamii. Msomaji usome vitabu vya Dostoïevski (hasa « Notes from the Underground ») au kitabu cha Melville kiitwacho Billy Bud, utaelewa jinsi uovu huo unavyojikita katika nafsi ya mtu, mbali na cheo chake na majukumu aliyo nayo katika jamii. Hapo msomaji nimetafsiri dondoo dogo la kitabu cha Dostoïevski ambalo linatudhihirishia wazi huo mchakato wa kupenda na kutaka kutesa na kudhuru :

« …Isitoshe binadamu huyo akikabidhiwa utajiri wote wa dunia, akipata maisha yenye raha starehe kupindukia, aidha akifurahia anasa zile za kuishi bila ya matatizo yoyote kiasi cha kwamba huishi katika hali ya shibe, na kweli binadamu huyo atakuwa hana kazi yoyote isipokuwa kulala usingizi mnono, kujipatia starehe na kula chakula kizuri chenye rutuba, yote hayo ya kuweza kumwepushia misukosuko ya aina yoyote katika maisha yake, basi iko siku binadamu huyo atakuwa hakosi kukupangia hiana na husuda, kwa hiari na raha zake mwenyewe, ili wewe mwenzake upate kuanguka. Isitoshe, anaweza hata kujinyima kula kuku kwa mrija na kufyonza sharubati kwa buruji, ili mradi hekima yake nzuri ipate kunywa kidogo uovu huo wa kuchukiza. Na kweli hekima yake ikikorogana na uovu huo itazidishwa na ujinga wa kutupwa. Lakini ujinga huo ndio atakaoung’ang’ania sana kwa sababu utamdhibitishia kwamba binadamu, na yeye kwanza,  amejaa utu. Kwani binadamu si binadamu tena kama tabia yake inatabirika ama kupimika kila wakati. Utu wa binadamu si kama ngozi ile ya ngoma mtu atakayeiwamba kabla ya kupiga ngoma ili apate ile sauti anayoitaka. Na hata hivyo, hata kama utamletea mtu huyo ithibati zote za kisayansi za kumthibitishia kwamba tabia ya mtu inatabirika, basi itakuwa haimtoshi. Kinyume na hayo, usishangae kumwona akifanya au akiendeleza ukaidi kwa kuwa atapendelea ubishi kuliko mwafaka. »

Raha ya kusikia kuwa umefanikiwa kukwamisha mradi fulani, ama umewahi kuudidimisha mpango wa kuhifadhi pori au msitu fulani mkubwa kwa kuuchomelea moto, mtaalamu wa taaluma zote za dunia, bado hajafahamu. Zile sayansi za jamii (sosholojia na antropolojia) hazina maana hapo kwa kuwa zinashindwa kuchambua maumbile ya binadamu. Hapa Afrika mashariki usifike mbali. Utembelee hifadhi zile za wanyamapori ambazo zinaleta faida kubwa katika nchi hizo husika na utajua husuda na uchoyo ni kitu gani. Si wanyamapori tu ambao wameangamizwa, pia ni mazingira yenyewe ambayo ni machafu, barabara zote ambazo zimeharibika, kwa kifupi miundombinu yote ambayo imefujika. Na wewe msafiri ukiongea na wahusika, wakina rangers, kuhusu janga hilo, basi utaambiwa kwamba wanyama wanajificha kwa sababu ya hali ya hewa au hujabahatika kuwaona. Kwa kifupi, uwongo mtupu. Lakini endapo una kipaji hicho cha kuweza kupima hisia ya mtaalamu huyo unayeongea naye, bila shaka hutachelewa kuonea jinsi anavyoifurahia hali hiyo, kwa sababu umekosa ! Si hivyo tu, kwani umehangaika, umetapatapa na umechoka. Kwa nini wewe upate kuwaona wanyama wale wakati wengine hawajapata hata kufika hapo ? Kwa nini ufanikiwe wakati mimi ranger sina kitu ? Na hali kadhalika…

                                 


                                


                                  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni