04/02/2018

Tafsiri au takriri ? Mfano wa Victor Hugo


Kazi za wanazuoni za siku hizi kuhusiana na tafsiri zimejaa maelezo na chambuzi ambazo hurudia yale yale yaliyokwisha andika zamani sana katika vitabu vingi vya wataalamu wa hapa na pale. Katika vitabu vingi vya leo, mara nyingi hakuna kitu kipya, ila namna zile za kuzusha baadhi ya hoja za zamani ndizo zinazoleta hisia kwamba tumepata dhana mpya. Lakini hakuna ubunifu wala uvumbuzi. Ni kama kufungua mlango uliokwisha kufunguka. Tukirudi katika vitabu vile vya kwanza ambavyo vilitangulia katika kuchanganua kazi ya kutafisiri, tutapata majina mawili maarufu : Friedrich Schleiermacher (1768-1834) na José Ortega y Gasset (1883-1955). Friedrich Schleiermacher alikuwa ni mwanateolojia kutoka Ujerumani na José Ortega y Gasset naye alikuwa ni Mhispania. Wote wawili waliandika vitabu vizuri sana kuhusu tafsiri ambavyo nimevitumia katika makala yangu ya leo ili kukosoa mchezo wa kuigiza wa Victor Hugo (1802-1885) uliotafsiriwa na Marcel Kalunga katika kiswahili. Kwa kifupi, nitaonyesha kwamba kitabu hicho cha Victor Hugo si tafsiri bali ni fasiri vue (au guni ?) au, kwa maneno mengine, aina ya ukariri wa sentensi.

                                                                         

Kwanza tubaini kwamba tunapotafsiri tunakutanisha lugha mbili. Kutafisiri si kuhamisha au kubeba mafungu ya maneno kutoka lugha hadi nyingine. Vinginevyo, kazi ya mtafsiri ingekuwa ni kazi ya kuli. Ingekuwa ni kazi ya mpagazi anayehawilisha kitu kutoka gunia moja hadi gunia nyingine. Kazi ya mpagazi ni kujihakikisha kwamba gunia hizo zinafanana kwa uzito, kipimo na ukubwa. Lakini lugha si magunia. Lugha zinatofautiana kwa kutoonyesha sifa moja. Kwa kifupi, kuna lugha mkubwa na lugha ndogo. Sababu ni kwamba kila moja imestawi, kutokana na historia na mazingira yake, kwa kufuata maendeleo ya kipekee. Hata lugha mbili ambazo zinafanana kwa kushiriki asili moja, kwa mfano kifaransa na kiitaliano, ama kilingala na kiswahili, basi kila moja ina upeo wake wa kuwasilisha maana ambao si wa lugha ndugu. Kwa maana nyingine, hakuna lugha iliyokamilika, kwa sababu kila lugha ina kimya zake, upungufu wake na utambulisho wake ambao pia ni dosari. Kama alivyoandika Victor Hugo :

« Lugha yangu imekoma kumaanisha pale pale ambapo lugha nyingine ya kigeni inaendelea kumaanisha. Jambo ambalo husemekana katika lugha moja halisemekani katika lugha nyingine. Katika lugha zote mambo mengi hayasemwi na mengine hayasemekani. »

Msanii mfaransa mwingine maarufu sana wa karne 20, kwa jina lake Paul Valéry, aliwahi kuandika : « Nina haja ya Mjerumani ili kukamilisha mawazo yangu ». Mfano wa kiitaliano na kifaransa utatuletea faida hapo katika tafakuri hiyo : kiitaliano kimetajirika sana katika nyanja kadha za usanii, ujumi na muziki, tangu zamani sana, angalau tokea karne 13. Kikilinganishwa na kifaransa, katika mawanda haya pekee, lugha ya kifaransa itaonekana imezidiwa kwa kiasi fulani. Haina ukamilifu huo wa kiitaliano. Isitoshe, kwa sababu Ufaransa na Italia ni nchi ambazo zilipigana sana zamani, mbali na kujenga urafiki pia, basi nchi hizo zimepeana na kukopeana msamiati mengi, hususan katika taaluma zile za ujenzi sanifu na sanaa kadha. Leo hii, asilimia kubwa ya maneno ya kifaransa katika istilahi ya ujenzi sanifu inatoka katika lugha ya kiitaliano.

Tatizo linaibuka wakati tunapotaka kutafsiri katika lugha ambayo si kufu ya lugha ile tunayoitumia kila siku. Mtu atashindwa kuingiza katika gunia dogo yaliyomo katika gunia kubwa. Mfano wa kifaransa na kiswahili. Lugha hizi mbili hazilingani hata kidogo. Hakuna usawa. Kifaransa ni lugha tajiri tukikilinganisha na kiswahili (na kiswahili ni lugha tajiri tukikilinganisha na kilingala). Kwa sababu ya historia tofauti kati ya lugha hizo. Mara nyingi huwa tunafikiri kwamba lugha ni chombo simulizi ama ongezi tu. Tunasahau kwamba pia ni miundombinu, pamoja na kwamba ni urithi ulioshikika. Kifaransa na lugha nyingine tajiri za dunia zimekuwa tajiri kwa sababu ya juhudi walizofanya watangulizi au waasisi wa zamani ya kale huku wakijitahidi kila wakati kuweka misingi madhubuti ya lugha hizo, ikiwa ni pamoja na kujenga shule, semina ya dini, majengo mbalimbali kama maktaba, kasri na makaazi ya wasanii, makampuni ya kuchapisha vitabu, maduka, taasisi mbalimbali, tasnia ya kutegemeza uhai wa fasihi, mavani maalumu kwa ajili ya wasanii wa zamani, makavazi na makumbusho ya kuhifadhi yale ya kale, na kadhalika. Itakuwaje tusawazishe lugha tajiri na maskini — ambazo hazina miundo hii ya kuimarisha lugha — kwa mujibu ya itikadi ya usawa ilhali watu wenye lugha hizo tajiri waliamka zamani sana wakajitahidi, kwa kujitolea na kutoka jasho jingi, kuiendeleza lugha yao ? Si kudharau yaliyojengeka katika lugha hizo ? Isitoshe si kudhalilisha juhudi zile ambazo bila shaka ni msingi thabiti ya kuendeleza lugha zetu — ziwe maskini ama tajiri — zikawa lugha bora katika sifa nyingi, kutoka ushairi hadi sayansi ?

                                                        

Mwanateolojia Schleiermacher aliwahi kuandika katika kitabu chake « Mbinu kadha wa kutafisiri » kuwa kuna njia mbili za kutafsiri. Ya kwanza ni kazi ile inayosahilisha lugha aliyotumia mwandishi ili msomaji apate kuielewa vizuri katika lugha yake. Kwa maana yake, mwandishi aliyeandika kitabu tunachotafisiri anachukuliwa kitikiti ili maandishi yake yatoholewe na msomaji asipate taabu katika usomaji wake. Imekuwa kama kwamba mwandishi, aliyeandika kitabu kwa kutumia satua na stadi za kisanii zisizo na kifani, basi alazimishwe kumnyepesishia msomaji lugha yake ili amkaribie… Tafsiri kama hii ni kama kupotoa na kuboronga maana ya kitabu cha mwandishi ili msomaji asiudhike wakati atakapokisoma katika lugha yake. Ya pili ni kazi ambayo, kinyume na ile ya kwanza, inajitahidi kulenga lugha ya msomaji na kuistawisha kila ibidipo, hususan wakati lugha lengwa inakosa msamiati au dhana zilizopatikana katika lugha chanzi. Ina maana kwamba tafsiri huwa ni aina ya ubunifu kwa kuwa mtafsiri hana budi kuzalisha upya baadhi ya dhana ambazo hazipo katika lugha lengwa. Hapo ndipo inapopatikana tafsiri kamili, kwa mujibu wa ufafanuzi wa Schleiermacher. Njia ya kwanza si tafsiri bali ni hawilisho ama, wakati tokeo la tafsiri si baya sana, ni zoezi la uigizaji. Kwa kifupi, ni ukariri wa sentensi lakini si tafsiri.

Mfano wa njia hiyo tunao katika tafsiri ya kitabu kimojawapo cha msanii Victor Hugo ambacho kilipatwa kutafsiriwa si muda mwingi nyuma. Nacho kinaitwa Michezo ya Mfalme kwa kiswahili. Mfasiri mwenyewe si msanii bali ni Profesa kutoka chuo kikuu cha Lumbubashi. Tafsiri iliyopatikana katika juhudi hizo hairidhishi hata kidogo. Ni jambo la kustaajabisha kwa sababu Victor Hugo mwenyewe aliwahi kutufafanulia jinsi mtafsiri anavyopaswa kutafsiri kazi ya fasihi. Kama alivyoandika, tafsiri bora ndiyo ile inayojitahidi kuyageuza matini chanzi ili mradi ipatikane matini huisho katika lugha lengwa. Katika zoezi hilo, mtafsiri hana budi kujihakikisha kwamba hajapoteza yale ambayo ni mihimili ya tungo aliloandika mwandishi. Victor Hugo tena anatukumbushia kinachotakikana katika juhudi hizo. Mtafsiri anapaswa kuenzi na kuheshimu unafsi (kf. esprit, kg. wit) wa mwandishi, kwa maana nyingine inabidi azingatie kipaji cha msanii, muono pamoja na mitindo yake. Isitoshe, katika vipengele vingine muhimu ambavyo mtafsiri hushurutishwa kuzingatia pia ni muktadha na kipindi kile alichokuwa anaishi mwandishi. Kufahamu muktadha huo kunachangia katika juhudi za mtafsiri za kufanikisha fasiri yake. Majina ya pahala pamoja na wahusika pia yanapaswa kutajwa kama yalivyofinyangwa na msanii mwenyewe. Victo Hugo alikazia kwamba matini yote yatafsiriwe kwa kadiri iwezekanavyo.

Kuna aina nyingi za tafsiri. Nimeshaandika makala machache penye blogu hii kuhusu mikabala ya aina mbalimbali katika mchakato wa tafsiri. Kuna tafsiri sisisi (HAPA), tafsiri fasiri (HAPA) na tafsiri haini (HAPA). Hapo leo sitaficha jinsi nilivyoudhika baada ya kusoma tafsiri ya Profesa Kalunga. Nina uhakika kwamba Michezo ya Mfalme si tafsiri bali ni takriri. Kama alivyodokeza Schleiermacher niliyewahi kutaja hapo juu, mtafsiri alisoma tamthilia ya Victor Hugo, kisha akatoa nakala nyingine, kwa kiswahili. Alifanya kazi ya kuli. Lakini katika upagazi huo, alipoteza maudhui mengi mno. Msomaji ukiwa na ustadi wa kusoma katika lugha mbili, kifaransa na kiswahili, utashindwa kuhisia ule unafsi wa Victor Hugo katika nakala ya kiswahili. Hupati dhana hiyo ya kuwa Victor Hugo, mbali na kuwa ni mtunzi hodari, pia alikuwa ni mshairi mahiri aliyekuwa amefungika kivyake kufuatana na uketo wa nadhari yake ya maisha yaliyomzunguka. Kinyume na hisia na dhana hizo unazotegemea kufikwa nazo, basi utajisikia umepata kitu kingine, yaani kitabu ambacho kimekolezwa ndani ya lugha ya kienyeji, hicho kiswahili cha Congo kiitwacho Kingwana, ambacho kinatumiwa na watu ambao hawana mionjo na mielekeo inayobebwa na tamthilia ile ya Victor Hugo. Lugha aliyoitumia Victor Hugo katika tamthiliya yake si lugha ya kawaida. Ni lugha ya mbunifu. Hivyo kazi angaliifanya mtafsiri si kusahilisha lugha ya Victor Hugo kwa ajili ya kukimu mahitaji ya wasomaji kwa kiswahili bali ni kuihuisha lugha hiyo katika umbo mpya, ule wa mchezo wa kiswahili. Ina maana kwamba mtafsiri amependelea kuwaendea wasomaji wake kwanza, kwa kujitazama kwingi, na kwa kuwabembeleza sana, katika lugha lengwa (kingwana) huku hatimaye akiwa amedharau fani na mitindo ya msanii mwenyewe. Matokeo yake ni kwamba mtafsiri ameidunisha tamthilia ya Victor Hugo. Mengi kutoka tungo ya kifaransa hayakutafisiriwa na mengineo yametafsiriwa vibaya au kwa kutumia maneno ambayo hayafai. Majina mengi ya kuonyesha hadhi ya wahusika, ama kutaja mahala muhimu ya Ufaransa hayakutafsiriwa (Bastille, Comte, Gargantua, courtisan, Seigneur, n.k.)

Tunajua kwamba katika tamthilia ama riwaya, na hilo ni kipengele kikubwa ambacho tunapaswa kukitilia maanani, kanuni za nathari huoana na mdundo wa hisia na ilhamu ya msanii. Tukiwa tumekata shauri ya kutafsiri fulani ama bin fulani, hatuna budi kwanza kusomea tabia na unafsi wa msanii mhusika ili tuwe karibu naye. Katika Michezo ya Mfalme, tunahisi kwamba tumesingiziwa, na jina la Victor Hugo linatumika kama nomino tu la kubandikizia utupu fulani. Hilo ni dhahiri katika upangaji wa kitabu chenyewe cha kiswahili. Ingawa kimetangulizwa na dibaji ya mchapishaji, hatuna hata kifafanuzi kuhusu wasifu wa Victor Hugo. Isitoshe, tunaambiwa kwamba alifariki mwaka 1855 ! Aidha, mchezo huo uliandikwa katika muktadha gani, katika jamii gani, yenye siasa gani ? Hatujui. Sina uhakika kwamba Afrika mashariki wasomaji wameshapata kusikia hata jina la msanii huyo. Ilikuwa ni wajibu wa mtafsiri ama mhariri kutoa angalau vichache. Si hundi na posho zilipatikana kutoka katika serikali ya Ufaransa ? Na sidhani kwamba Mswahili msomi ambaye amekubuhu ndani ya fasihi ya kiswahili, angekubali diwani ya mashairi ya Shabaan Robert itafsiriwe katika lugha nyingine ya kigeni, lakini kwa kutumia msamiati na matamko ya kawaida — lugha inayoongeleka ndani ya kibanda cha wavuvi — na katika kitabu hicho msomaji asiwe na hata chembe cha taarifa juu ya maisha ya mshairi huyo.

Kutafsiri ni kukaribisha, ni kuitikia hodi iliyobishwa mbali, ng’ambu, katika nchi ya kigeni. Tafsiri bora huonyesha dalili ya ukarimu. Mgeni anaomba kuingia upenuni huku akibeba ugeni wake. Mtafsiri, ambaye ni mshenga au mjumbe, kazi yake ni kumkaribisha kama alivyo, si kumwambia « wee mgeni vaa kama tulivyovaa sisi kwanza ! ». Mgeni huyo ajisikie amependwa. Akishajua kuwa amependwa, watu watapendana. Wakipendana, wataathiriana. Sidhani kwamba, katika dunia yetu ya kuchukizana kama ilivyo siku hizi katika mawasiliano baina ya Afrika na nchi za magharibi, sidhani kwamba namna hiyo ya kutafsiri itakubalika. Tukipekua pekua haraka haraka jinsi baadhi ya watafsiri walivyotafsiri tungo mbalimbali za waandishi maarufu wa Ulaya, mtu atasikia mara moja kwamba kina Shakespeare, Gogol, Molière, na sasa Victor Hugo wameswahilishwa ilhali usanii wao ungalichangia kuingiza ugeni fulani katika miundo na fani za fasihi ya Waswahili. Badala ya kutafsiri Shakespeare, Mwalimu Nyerere alijitafsiri kwanza, alijipeleka mbele, alitangaza umimi wake, alikuza uzalendo wake, alijenga siasa yake, hadi kutuletea kichekesho kikubwa. Eti Shakespeare ameandika kitabu kiitwacho Mapebari wa Venisi ! Kinyume na mchakato huo wa kujiangazia na kujivuna, tunaona kwamba vitabu vingi vya bara la Afrika, kama kile maarufu cha Tutuola — na mimi hapo nakumbuka tafsiri ya ajabu ya kitabu chake maarufu The palm wine drinkard (1952), iliyofanywa na Raymond Queneau katika kifaransa —, ama vitabu vya Ahmadou Kourouma, vyote vimeingiza semi za shani katika lugha ambako vilikokwenda kutafisiriwa. Mimi nimefurahi sana niliposoma vitabu vya Kourouma na jinsi alivyoboronga kile kifaransa chetu. Kwa sababu ya mchango huo, kifaransa chetu kimebadilika. Kisha kimepanuka, kimetajirika. Nashukuru sana.

                                                                            

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni