19/04/2018

Husuda yaua kwa jicho la wivu


Hapo Uganda, magazeti na mativi yamefikwa na fadhaiko kubwa. Simba kumi na moja wameuawa katika mbuga ya Queen Elizabeth kinyume na sheria. Lakini wahalifu wamekamatwa. Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kwamba wametumia sumu. Matokeo yake, mapaparazi wa Majuu wamechanganyikiwa. Mzungu hapo amenuna, ameghadhibika. Sijui Guardian (hapa), The Independent (hapa) na magazeti mengine ya Yuke na Unyamezini, wamekuja juu huku wakiripoti kuwa unga umezidi maji. Ole wao ! Eti walikuwa ni simba wa mwisho katika mbuga hiyo. Kwa nini wafanya kazi wa mbuga hizo wanadorora ? Watu hawajui kwamba wana changamoto kubwa na bila shaka hadi leo "wahusika hawa wenye jukumu zito" wamekaa chonjo. Lakini si unajua, shemeji yangu amenisumbukia siku ile. 

Mzungu ndiye anayependa wanyamapori, ndiye anayeleta mshiko. Ndio ubwege wake, utamaduni wake, maumbile yake, sijui dhana gani ni noma hapo. Mimi sijali. Kwa sababu kote duniani tunashuhudia ujinga wa binadamu, isipokuwa Afrika. Kwa kuwa Afrika si kizimba cha wanyamapori, si ndiyo ? Afrika si bara nyeusi, ni bara ya ubunifu mkubwa, ni bara ya uvumbuzi wa kila siku, ni bara ya wana sayansi wa hali ya juu ambao, hapo ndipo tunaomba ripuripu, watatusaidia sisi binadamu tupate maendeleo endelevu ya aushi milele katika sayansi na teke-linalokujia haraka haraka. Mashaallah !

Mimi hapo naomba tuzifunge kabisa, tena kwa haraka iwezekanavyo, mbuga na hifadhi zote hizo za kikoloni. Ya nini hizo ? Tumechoka na malodji ya fahari fahari, mashangingi yanayopita kwa kasi katika vijiji vyetu vya nyumba zetu za kujiinamia mbavu za mbwa. Kwani bado wazungu wale wana muono wa kikoloni ? Uromansia umekwisha sasa, mambo ya tomasa tomasa hayo ni ya kizungu. Sisi mtazamo wetu wa ado ado, falsafa yetu ya uduara, si ndiyo, ya tusogezeane vigoda tupige matonge. Msomaji angalia picha zifuatazo za kina mshkaji walivyochangamka kishenzi. Raha tu, raha ya maovu… "Utamaduni wetu umefufuka, usikonde braza, wan lov". 

                                                   

                                                                                                                             Picha hizi, Courtesy@ Sekororo News Hapo

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni