06/04/2018

Mashairi mawili niliyoyapendaNishike Mkono

Iwapo macho yako
yanaangaza huku na huko
   miaka kwa miaka
yakitafuta upeo uliotuponyoka
yakiangalia vioo vilivyopasuka
vilivyoacha
  vivuli vilotawanyika
              na vigae moyoni kujifumika

basi,
        hebu nishike nami mkono
        unambie safari ndiyo hino
              matata yajapo
              zinduko lijapo
              faraja ijapo
                       niwe pamoja nawe
                       pamoja tu
                               mkono kwa mkono

Alamin Mazrui

Dikteta

Kama wajiona ni wewe pekee
Uwezaye kufikiri
Ulikufa karne nyingi zilizopita.
Kilichobaki ni wako mweweseko.
Wale uliowakemea, uliowaweka ndani
Uliowadhulumu na uliowaua
Mawazo yao sasa milizamu
Ambamo watoto hucheza kwa furaha
Na kunawa shombo uliloliacha.

Madaraka ni ndoto isiyotegemewa.
Ni kuvaa kofia juu ya gari wazi
Lendalo mbio kuvuka mto wa haki
Ambao daraja lake limechukuliwa
Na mafuriko ya sheria ulizovunja,
Ambalo breki zake ni roho za watu
Na matairi yake ni mafuvu manne
Ya wale uliowaita vichwangumu
Haini namba wani wa fikra zako.

E. Kezilahabi

Si rahisi kubainisha kiini kile cha hisia niliyo nayo wakati wa kusoma mashairi hayo. Upendo hauna mantiki. Huenda mashairi hayo yamenishtua kwa sababu yameniletea aina ya chamko moyoni mwangu. Pengine ndiyo inayoitwa fahamu fiche, ama uelewa bwete. La msingi ni kuwa msomaji hana haja ya kujua maana ya vina, mizani, mshororo na kadhalika ili kupenda ushairi. Kusoma shairi ni kuingia katika bahari ya hisia kwanza, si kujitosa katika dawe la kanuni na sheria. Ndio maana sisi tuliokuwa tumepata bahati ya kusoma ushairi shuleni bila hata kuzingatia kanuni zile za ushairi, tungali tunapenda ushairi — na mimi hapo nilipo nimeshaingia katika uzee. Hadi leo ningali nayajua mashairi yale niliyoyasoma na kujifunza shuleni. Na mengine mengi nayatoa kwa ghibu wakati nakutana na baadhi ya wenzangu wapenzi wa ushairi. Na lipo moja, miongoni mengi mazuri sana, ambalo lilitungwa na Marie de France karne 12. Ningali nalijua kwa moyo, pamoja na mengine mengi, ikiwa ni pamoja na shairi zuri pia liitwalo Kitu kizuri…

Uswahilini, tangu 1974, ushairi huru upo. Si haba. Na unapendeza. Ingawa maafande na makoplo wa kambi ya jadi wanaendelea kujibanza. Wangali watatia chonjo, bila shaka. Lakini watakoma, kama walivyokoma wenzao katika jamii nyingine. Kwani mgogoro uliopo Afrika mashariki siku hizi si wa kienyeji tu. Kwingine ulishatokea, nadhani katika mapokeo yote. Kupatikana kwa mwafaka katika utanzu huo wa ushairi kungekuwa ni dalili ya ugonjwa fulani. Kinyume na hayo, marumbano ni chocheo. Ni ishara ya amali fulani. Hakuna lugha isiyokuwa na uhai.

Ninapoona jinsi mgogoro ulivyopamba moto katika jamii ya washairi wa kiswahili — baina ya wanaojitia urasimi na wanaojitia usasa — nashindwa kujizuia kukumbukia mgogoro ule mwingine uliotokea kwetu karne 19. La kushangaza ni kuona kwamba wahusika wa hapa na pale wanaabiria kauli zile zile. Si Ulaya, si Afrika. Nakumbuka kauli ya mshairi maarufu Victor Hugo (1802-1885), mwaka 1834, alipokuja kuchokoza « warithi » na washairi wa jadi waliokuwa wanatunga mashairi yenye mizani 12, huku akisema « tayari nimekomesha umbumbumbu wa ushairi wa jadi ». Hatimaye wengi walimfuata — ingawa palizuka vurugu kubwa — wakina Charles Baudelaire (1821-1867) na Arthur Rimbaud (1854-1891), nao wakiwasilisha shani na ubunifu mkubwa. Iko siku mageuzi yaliyoletwa na washairi hawa yakapuuzwa yakachukuliwa na vizazi vile vilivyokuja baadaye kuwa ni urasimi. Wakina Mallarmé (1842-1898) na Apollinaire (1880-1918) nao pia wakaibua muundo na kanuni nyingine. Uswahilini vilevile, iko siku wakina Kezilahabi na Alamin Mazrui watakuwa wamepitwa na wakati. Muhimu ni kukumbuka na kupenda.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni