25/05/2018

Kumbe mashujaa Afrika wapo : Siti Phyllis Omido kutoka Kenya


Sisi tunaozidi kukimbiwa na ujana huku tukiingia katika bahari chafu ya heshima — kwani heshima isiyokuwa na elimu si jaa ? — kila siku tunainukia dunia inayotuletea shani na miujiza ya kutusaidia tujisahihishe, tujirekebishe na tuamini kwamba kweli maisha bora yanaweza yakapatikana. Sahihi yatapatikana ikiwa binadamu akubali kujitolea na kuacha tabia yake ya uzembe, uvivu na ujinga. Wanadamu wa hapa na pale, katika nchi za magharibi pamoja na nchi nyingi za dunia, wamejenga tajiriba kubwa sana, tangu zamani, katika kuhifadhi, kutetea na kulinda mazingira yetu hadi wengi katika wao hawana hata hofu ya kujiponza kimaisha. Hapo sitataja wana harakati wengi mno wa nchi za magharibi — kupitia mashirika maarufu kama Greenpeace, See Shepherd, IFAW na kadhalika ambayo kila siku hupigania haki ya uhai, hususan katika sekta mbalimbali ya utetezi wa maliasili ya dunia yetu. Bali nitapenda kutaja jina la siti Phyllis Omido kutoka Kenya.

Afrika si aghalabu kupata mwana harakati mwenye ujasiri na uzoefu wa kina katika kuimarisha usalama wa mazingira kwa jumla. Uzoefu huo unataka mtu awe na elimu ya kutosha katika sekta hiyo, kitu ambacho shule za nchi za Afrika hazijapambana nacho, seuze Vyuo Vikuu ambapo mwana vyuoni shida haoni. Hakuna nafasi, katika mitaala ya shule za nchi hizo, kwa taaluma ama ujuzi unaohusisha swala hilo la utetezi wa mazingira. Licha ya sayansi zile za ikolojia kwa jumla. Isitoshe, inabidi mtu awe na upeo mkubwa wa akili tambuzi katika taaluma ambazo zinataka kushughulikiwa kwa umahiri mtambuka. Mara nyingi msomi ni mtaalamu wa hoja moja tu wala hana uelewa wa kutosha wa hoja nyingine ambazo, kutokana na hali jinsi misingi ya uhai ilivyojengeka, zinataka kubebwa kiujumla. Hakuna bayolojia katika mazingira bali kuna mfumo ikolojia usiofahamika ila kwa kujenga mikabala ya aina nyingi ambayo imeegemea juu ya bayolojia, itolojia, na sayansi nyingi za kimaumbile. Zote zinakamilishana.

Women Activists, Fred Mutebi (hapa)
Kutetea mazingira si lazima uwe na ujuzi mwingi. Maarifa yanafaa. Pamoja na hekima. Na kwa sababu ajali haibishi hodi, nadhari ndiyo sifa kubwa itakayombainisha mwana harakati katika watu wote. Yeye hangojei tukio bali analitabiri. Ndizo sifa hizo tajika ambazo bila shaka zilimsukuma Siti Phyllis Omido katika kutetea haki ya watoto ambao waligundulika kuwa na kiwango kikubwa cha madini ya risasi katika damu baada ya viwanda vya kuyeyusha risasi viliposhutumiwa kumwaga madini hayo katika mito ya kitongoji duni cha Owino Uhuru, Mombasa. Kiwango hicho cha madini katika damu ndicho kilichosababisha mwanawe na watoto wengine wa mtaa huo, pamoja na wengine wa sehemu nyingine ya Kenya, kupata maradhi mbaya ambayo si rahisi kutibu. Juhudi za Siti Phyllis Omido zimefanikiwa pakubwa, kwanza kuwania haki ya watu maskini ambao huishi kwa dhiki na mashaka katika mazingira yasiyokuwa na miundombinu ya msingi. Na bila shaka, kama ilivyo katika jamii ambapo makabaila ndio wamebeba sheria mfukoni mwao, huku wakiwa marungu mikononi, wanaharakati hawa huteswa, huonewa kupita kiasi, kwa kadiri wanavyoshikilia utetezi wa haki ya binadamu.


Alifanikiwa pia kwa sababu alikabidhiwa tuzo ya mazingira ya Goldman (HAPA) na kwa sababu ya juhudi zake katika kuanzisha shirika ama asasi isiyokuwa ya serikali — ambayo inaitwa Center of Justice, Governance, and Environmental Action (CJGEA, HAPA), shirika linalohusikia usalama wa kimazingira hasa katika maeneo yaliyo karibu na viwanda. Hiyo ndiyo hatua kubwa inayoonyesha kwamba bidii na ari ya kufanikisha maendeleo kwa kutumia mbinu zilizokamilika — ambazo zina uhalali mkubwa —ni vigezo vya maana za kudhihirisha kwamba zihi pamoja na amali ni mihimili mikubwa katika jamii. Kinyume na hizo, uzorotaji, uzohali na uchoyo huwa ni saratani sugu ambayo mara nyingi huchamka katika mazingira ya uchafuzi unaozidi kuzikumba nchi zote za Afrika. Msomaji asiwe bwege kiasi cha kutozingatia kilichowahi kutokea hapa na pale duniani — huku akidhani kwamba Afrika ni bara tofauti na sehemu nyingine za dunia. Siti Phyllis Omido ni mwanzilishi Afrika. Lakini maafa aliyokumbwa nayo, yeye na jamaa zake katika mtaa wa Owino Uhuru, si jambo jipya. Yote yameshatokea, katika nchi nyingi za dunia, nisitaje maafa ya Bhopal na Tchernobyl (HAPA), ambayo yalisababisha maangamizi makubwa mno. Hapa penye bara ya Afrika, tuko njiani, uharibifu na uchafuzi umeshanyemelea. Iko siku, bila shaka.Hakuna maoni:

Chapisha Maoni