08/06/2018

Jando (1) : ngariba amefika

Katika enzi za kale, katika sehemu nyingi za Afrika, watoto walipokuwa wametimia umri fulani walikuwa wanapelekwa jandoni. Kwa kiswahili, tunasema kwamba watoto wanakaa kitako, ama kuwa wanakwenda kuhitiniwa ama kutahiriwa. Kwa kifupi, Uswahilini, watu husema kwamba wasungo wanakwenda kwenye ikidi. Siku hizi jando, kwa maana ya jando ya jadi, imekufa. Mimi mwenyewe na mwenzangu Ryo Nakamura kutoka Chuo Kikuu cha Fukuoka Japan, tuliwahi kuhudhuria shughuli hizo ambazo, wakati ule, zilikuwa zinahusisha watoto wa Kilwa na vijijini vyake. Katika shughuli hizo kulikuwa na hatua kadha ama tuseme vidato vichache vya kutimizia tokea siku yenyewe ya tohara hadi siku ya kukuwira yaani kurukwa kwa jando. Kwa jumla, watoto walikuwa kwanza wanatahariwa na fundi anayeitwa ngariba. Ndiye aliyekuja kutahiri wasungo kwanza kabla hawajafikishwa porini katika utagala (kumbi kwa kiswahili cha kamusi) ulioongozwa na nyakanga. Nyakanga ni kiongozi ambaye, kutokana na ufundi wake katika mambo ya uganga, hutoa mafunzo mengi yanayoambatana na maswala ya itikadi, usuli, tabaka la kijamii na mawasilianao ya kijinsia. Ndipo utagalani wari walipotawishwa muda mwingi, takriban miezi miwili, huku wakifundishwa jinsi vile wanavyopaswa kuzimudu asasi muhimu za jamii, ikiwemo lugha, maadili ya kienyeji na mambo mengineyo.

Katika vichapisho vya leo na vya siku zijazo, nimeamua kuchapisha vichache tu, vile vya kazi yetu tuliyofanya na mwenzangu Ryo Nakamura, ambaye ndiye aliyepiga filamu. Katika video hizi ndogo, tunaona jinsi ambavyo jamaa wote wa kijiji wamekusanyika uwanjani — katika mzunguko wa kijiji —, huku wakiwa wamepangana vizuri ili kumlaki ngariba. Ngariba yupo katikati, kivulini kwa mti, anaimba mwimbo uitwao « Alimanguto », huku akitegemea kufupwa au, kwa kiswahili cha mjini, kutunzwa. Watu wanamwendea, wanatoa senti chache, kisha wanarudi katika msururu wa watu. Katika nyimbo nyingi ambazo huimbwa, tunazikuta hizi zifuatazo :

1- Anapoingia Ngariba kijijini, siku moja kabla ya shughuli ya kutahiri, mwimbo huo unasikika :

Ori ! gae gae karitira
Ori ! gae gae karitira
Na mwari paranda

Ori ! Gaegae (buibui mkubwa sana) kaingia
Ori ! Gaegae (buibui mkubwa sana) kaingia
Mwari atakwenda porini

2- Asubuhi mapema, siku ile ya kutahiri, nyimbo hizi huimbwa :

Pambano ndipo pao
Ndipo pao unyago
Ndipo pao unyago

Hapo ndipo penyewe
Hapo ndipo shughuli

3- Kisha penye uwanja pale :

Ngariba :
Alimanguto leo !

Kiitikio :
Alimanguto mwanangu mwanja
Kisimani utamtuma nani ?
Kutuma utantuma nani ?
Kuchapa utanchapa nani ?
Kutukana utantukana nani ?
Kumfyonya utanfyonya nani ?

4- Anapokwenda kutahiri, ndipo ngariba anapoimba :

Tukimure kincheni nnore
Nnore tukimure kimasimba

Tuchapie, tucheze, mkaone
Mkaone tunacheza kisimba

5- Kisha :

Mwanjenu mwanja, mwanja
Nyaura malawi

Mwenzenu naondoka, naondoka
Wari, natangulia !
                                                                                 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni