10/06/2018

Jando (2) : ngariba anatayarisha mambo

Kama tulivyoandika katika kichapisho cha kwanza (jando 1), wasungo wanatahiriwa porini, pahala ambapo si mbali kutoka kijiji. Huko ndiko wanaume pekee wanapojikusanya. Mwenye shughuli, ngariba na wafuasi wake huzunguka kitanda cha mayowe ambacho kimefunikwa na mkeka. Kitanda hicho kitakwenda kutumika tena porini penye utagala ambapo nyakanga atakilalia. Kabla ya wasungo hawajafika, kuna kaida na kanuni mahususi ambazo zinapaswa kutekelezwa. Ni hatua ambazo zinaonekana wazi katika video ya kwanza. Tunaona kwanza jinsi msaidizi wa ngariba anavyotayarisha jogoo yule ambaye atasogezwa kwenye mvungu wa kitanda ili kuhakikisha kwamba hakuna uhasidi. Huyo jogoo huchinjwa endapo mvungu huo haukaliki. Kisha ngariba anaomba ruhusa ya kutahiri. Ndio maana anawaita washiriki na wahusika wote wa shughuli. Hapo tunaelewa dhahiri kwamba tupo katika mapokeo fulani ya jando, ambayo yanaitwa, katika vijiji vya Kilwa, tarehe ya kina ncheni. Hiyo jando ni ya watu wa pwani tu ambao hufuata mapokeo ya Waswahili. Mbali na mavazi ya ngariba — kilemba na joho — na vifaa vyake — kipenga, kisu na mkoba wake — kitanda pia ni kipengele kikubwa cha jando ya kiswahili. Tofauti na bara, hususan katika tarehe ya ngariba wa vijiji vya Ngindo, ambapo mafundi wa tohara huvaa njuga, shanga na ngozi ya chui na hujipaka rangi nyeupe ya kipaji inayoitwa ungigo. Pia, ngariba wa bara hawatumii kipenga bali firimbi. Isitoshe, hawatumii kitanda bali wanatahiri chini, juu ya mkeka. Katika sehemu ya pili, tunasikia ngariba anavyoita wakuu wa nasaba zenye maana katika jamii ya kiswahili, mathalan ni Washirazi, Wamalindi na Masharifu. Wao ndio wanaobeba haki ya kuhalilisha shughuli hiyo huku ngariba akikabidhiwa kisu kutoka mwenye shughuli ambaye ni mzazi wa chando (mtoto wa kwanza atakayetahiriwa). Hatua hiyo ya mwisho kabla ya kutahiri inafuatwa na dua la kiislamu.
Hakuna maoni:

Chapisha Maoni