19/06/2018

Jando (3) : kutahiri


Ngariba yu tayari kutahiri. Amekalia kitanda cha mayowe huku akisubiri kuletewa wasungo waliofika porini. Kila msungo hubebwa mgongoni kwa mrombo huku akiwa amefichwa gubigubi. Mrombo ni somo ambaye atamshughulikia mwari katika vipindi vyote vya jando, kuanzia hatua hiyo ya tohara hadi mwisho wa jando, wakati wari wanapotoka utagalani.

1- Kabla ya watoto hawajafika penye shughuli, kwanza warombo wanazinguka nao uwanjani kwa kijiji, mara tatu. Katika mzunguko huo, kuna mwimbo unaoimbwa, yaani mrombo mmoja anaimba, halafu anaiitikiwa na watoto kama ifuatayo :


Ainamire koti koti
Koti koti nguruwe

(ama : warinamira kotikoti nguruwe)

Yaani, watoto wanainamia kama nguruwe

2- Kisha, watoto wote wanabebwa kuelekea porini penye shughuli huku wakiimba :


Wana nchini mwanja,
Wana nchini mwanja,
Mwanja kunyakura maturi tuukee !

Maana : 

Wari twend' zetu
Tuchukue wari tuondoke

3- Kuna mwimbo huo pia, wakiwa wanasubiri kutahiriwa :

Munatukonga micheni nyie
Munatukonga micheni nyie
Wari wakiwa haba
Wari wakiwa haba
Na heri tutaire ndopa nkirora kindu lero !

4- Chando huletwa kwanza. Hapo penye video tunaona vizuri ngariba anavyotahiri. Wasaidizi wake wakiwa wameshamdhibiti mtoto, tayari ngariba hushika vifaa vyake. Katika mkono wake wa kushoto hukamata kijiti kiitwacho nsira. Matumizi ya nsira yanaonekana wazi katika video. Inamsaidia ngariba kulishikiza vizuri zunga la mtoto kabla ya kulikata. Wakati huo huo, wanaume wanaendelea kuimba kasida.
5- Katika hatua hiyo, watu hawafichi habari za matusi. Endapo mtoto amefikishwa kwenye kitanda chenyewe huku akidhihirisha kitu cha ajabu, ngariba ndipo huimba nyimbo zifuatazo : 

Kundonde kumiwili
Kokoro

Maana yake :

Porini mumeziba (mna miti mingi)
Ni giza

(yaani mtoto ameshaota mavuzi)

Ikiwa ngariba amemshtukia msungo ana tupu ndefu, ndipo anapoimba :

Mkunyanga hauna ndambi ngwerere

Maana yake :

Mkunyanga (mti fulani) ni mrefu, hauna matawi, umenyoka 

6- Akiwa anaendelea kutahiri, wakati mwingine ngariba anaimba nyimbo hizo :

Wamalindi wambenda wambenda
Washirazi wambenda wambenda
Washirazi wambenda wambenda
Nakupenda niki kanifurira
Ntari na nsiwa kindu lero

Maana yake :

Wamalindi wananipenda
Washirazi wananipenda
Wamenifulia kisu
Kisu na chuma, kitu leo !

7- Baada ya kutahiri, ngariba na wafuasi wake wanatakiwa kuimba mwimbo mwingine ufuatao, huku wakicheza ngoma ya kina ncheni, yaani mchezo wa kisu. Kisu (ntari) cha ngariba huinuka juu na wafuasi wake hucheza (zamani msondo ulipigwa wakati huo, cha kuwaarifu wana kijiji kwamba shughuli imekwisha). 

Simba akira nyama
Sikia chingurumo

Simba amekula nyama
Sikiliza ngurumo wake 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni