23/06/2016

Baadhi ya maswala aliyeniuliza rafiki yangu wa zamani "Yusuf" kuhusu kusilimu

Yafuatayo ni baadhi ya maswala aliyoniuliza rafiki yangu Yusuf niliyewahi kukutana naye Unguja miaka ishirini nyuma. Nilipokutana naye wakati ule, Yusuf alikuwa ni Mwislamu ambaye alijisilimu alipofika Unguja miaka tisa nyuma. Yeye alikuwa ni mwananchi kutoka Rwanda. Tulipokutana tena wiki mbili iliyopita nilipokwenda Rwanda, kwa kuwa ndiko aliporudi hivi karibuni kustakimu, nilishangaa kugundua kwamba amerudi katika Ukristo. Kwa kuwa Yusuf alikuwa Mwislamu msalihina na mbobezi katika kusoma na kupima maandishi matakatifu, nikaamua kumhoji tena — kama nilivyofanya miaka ishirini iliyopita (nikaandika makala hii hapa, kwa kifaransa) — kuhusu maana ya uamuzi huo naye akanitayarishia maswali haya yafuatayo ambayo yalikuwa yakimbana tangu zamani. Haya ndiyo yaliyomsukuma arejee katika dini ya Ukristo. Ni imani yake ambayo mimi mwenyewe sina budi kuiheshimu.

       1. Je, ungeamini chama kinachokataza makada yake wasitoke katika chama hicho na kuamini itikadi nyingine wakishatoka ? Kama Mwislamu hukatazwa kutanasari, je kwa nini na sisi tuiamini dini ya Uislamu ambayo inatesa na kuua wale wanaotoka katika Uislamu ?

2. Kwa nini wengi duniani wanatoka katika imani ya kiislamu ilhali wanajua kwamba kitendo hicho kinaponza maisha yao ?

3. Inasemekana kwamba mtu hawezi kukosoa Kuran kama hajui kiarabu na maana yake. Ikiwa ni hivyo, wengi katika Waislamu husoma Kuran huku wakiwa hawajui maana ya wanachosoma. Je, si kufuatilia na kueneza dini ambayo haieleweki ?

4. Inajulikana kwamba kiarabu cha Kuran ni lugha takatifu isiyo na hitilafu yoyote. Hivyo kwa nini Kuran imejaa maneno ya lugha mbali mbali, ikiwemo kihabesha, kiajemi, kilatini, kiyunani na nyinginezo ?

5. Lugha ya Kuran inachukuliwa haina dosari wala upungufu kwa sababu ni maneno ya Allah. Hivyo kwa nini sentensi nyingine hazina mantiki wala mizani ? Au Allah alitunga mategu ?

6. Lugha ya Kuran inadhaniwa ni lugha yenye mantiki. Je, kwa nini aya nyingi hazina mizani ? (Yusuf hapo aliniambia nisome 4.78-79 ; 6.148-149 ; au tulinganishe 2.47 na 5.18 au 35.24 na 25.51) Na kwa nini Mtume Mohamed alishushiwa aya ambazo, kutokana na sheria ya ubatilifu (naasikh wa mansuukh, kwa kiarabu), zinachukuliwa zimepitwa na wakati ?

7. Kuran inasema kwamba Maryam ni mama ya Yesu. Ikiwa ni hivyo, nani atakubali kwamba pia ni ndugu yake Aaron na Musa (19.28) ? Ama kweli Kuran inazungumzia Mariam ambaye ni ndugu yake Aaron na Musa ambao waliishi karne 12 kabla ya Yesu !

8. Kuran imetafsiriwa katika lugha nyingi duniani, ikiwemo lugha ya kiengereza, na Kuran hizo huhalalishwa na mamlaka makubwa ya kiislamu duniani kote. Je, kwa nini mtu asiye Mwislamu akitokeza akitaka kukosoa Kuran kwa kusoma tafsiri hizo, mara huambiwa kwamba tafsiri anayeitumia si sahihi ?

9. Kwa nini Waislamu wengi husema kwamba mwari aliyebaleghe ndiye pekee anayestahiki kuozeshwa wakati Kuran husema kwamba hata kigori anafaa ? (65.4 ; 33.49)

10. Je, mahaba baina ya mwanamme mwenye miaka hamsini na tatu na kigori mwenye umri wa miaka tisa kweli yanazingatia maadili na heshima ya binadamu ?

11. Kwa nini dini ya Uislamu ni dini pekee inayoshambulia dini nyinginezo ?

12. Je, Allah alitizamia migongano na vita baina ya Wasunni na Washia zilivyoibuka baada ya kifo cha Mtume Mohamed ?

13. Kuran inazumgumzia pombe kuwa ni aina ya kifundiro cha Shetani. Hivyo kwa nini Kuran inasema kwamba pombe itapatikana kwa wingi na kutiririka kama mito peponi  (5.90-91 ; 13.4 ; 47.15) ?

10. Kisayansi kunywa pombe kwa kiasi kidogo inachukuliwa ni aina ya dawa inayotunza moyo usipate fadhaiko na shtuko, na inayokinga mwili usipate kisukari na ganzi ya aina mbalimbali. Hivyo, kwa nini Allah imekataza pombe badala ya kupanga matumizi yake ?

11. Mtume Mohamed anadai kwamba maji ya zamzam ni aina ya tiba kuu inayotibu maradhi zote. Je, kwa nini maji haya imejaa kemikali nyingi kama vile asenia, nitrati na bakteria nyingine mbaya ? Soma HAPA.

12. Inaelekea kwamba dunia katika Kuran si tufe bali ni kama bamba la chuma au kitu bapa (Kuran inasema « zulia »). Lakini kama inajulikana ni tufe kweli, kwa nini Waislamu huswali kuelekea mashariki au kaskazini kutegemea walipo duniani wakati masafa yaliyo madogo zaidi yapitia ndani ya dunia tufe au kwenda kupitia ncha za dunia ? Au Allah hakujua kwamba dunia ni aina ya tufe ?

13. Mwislamu anapaswa kuswali kuelekea na kukabili Makka huku ikiongezwa kuwa kutofanya hivyo ni kukufuru Mungu. Je kweli kitendo hicho kina maana ikiwa tumejali kwamba dunia ni tufe ? Vyovyote vile, kuswali ni kuikabili NA kuipa kisogo Makka !

14. Kwa nini Allah hakupatunza pahala patakatifu « Kaaba » kila paliposhambuliwa mandhali ni pahala patakatifu ?

15. Kwa nini Waislamu wanaendelea kuzingatia itikadi ya kipagani inayowashurutisha waizunguke Kaaba mara saba kwa kufuata mzunguko unaokwenda kinyume na ule wa saa ?

16. Kwa nini Mwislamu mwenye hadhi na cheo nyingi hulindwa na doria nzima anapokwenda Makka wakati Mwislamu wa kawaida naye huachwa bila mlinzi ?

17. Huko Makka mamia ya watumishi hutumikiwa kila siku ili kusafisha maabadi ya Kabba. Je, kwa nini Allah anawaruhusu njiwa na ndege wengine kudondosha mavi juu ya pahala patakatifu ?

18. Kwa nini Allah anaruhusu watu wa damu moja, kwa mfano ndugu « simba kwa simba » kufunga ndoa wakati ndoa kama hii inajulikana wazi kwamba huleta madhara ya kijenetekia ? (4.23)

19. Mwanamme akitaka kumwacha mkewe hutamka « talaka » mara tatu, wakati mwanamke naye akitaka kuachana na mumewe anapaswa kujitetea mahakamani mbele ya hakimu mwanamme. Je, mchakato huo kweli ni haki ?

20. Katika Uislamu, mwanamke ambaye aliwahi kubakwa lakini hana shahidi wa kiume, mara nyingi hushtakiwa kwa hatia ya uzinifu. Je, hiyo ni haki ?

21. Kufuatana na sheria ya kiislamu, wazazi wa watoto ambao walishtakiwa kwa hatia ya uzinifu wanapaswa kuadhibiwa na kupigwa mawe. Hivyo Allah anapendekeza watoto wawe mayatima (wakati Kuran inasema kwamba haipendezi kuokota na kulea watoto waliotupwa (33.4)) ?

22. Mwislamu anajuaje kama Jibril aliyeongea na mtume Mohamed alitumwa na Mungu wala si Sheitani ?

23. Mtume Mohamed na wafuasi wake waliwaua watu zaidi ya mia saba wa kabila ya banu kuraiza, nao walikuwa wazee kwa watoto, mwaka 627. Je, unafikiri kwamba ni mfano wa kufuata ?

24. Katika Kuran, kuna aya nyingi zinazosema kwamba Mtume Mohamed alikuwa si mwenda wazimu. Kwani watu wengi walikuwa wanamchukulia vile wakati ule ?

25. Kwa nini Waislamu wengi wanakataa kwamba Mtume Mohamed alikuwa hupenda vigori wakati « hadith » nyingi zinakubali wazi kwamba alikuwa na tabia hiyo ? (hadith za Bukhari, Abu Dawud na Tabari)

26. Kama maisha ya Mtume Mohamed ni mfano wa kuiga, je kwa nini wengi katika Waislamu ambao wanajitahidi kumwiga wameonekana ni hayawani wenye ukatili mwingi (huku Yusuf akitaja mashambulio mengi ya hivi karibuni) ?

27. Kwa nini Allah alisubiri miaka mia sita ili kukata kauli ya kwamba Yesu hakusulubiwa juu ya msalaba ?

28. Kwa nini Mwislamu hupendelea kutumia dawa ya kimagharibi kuliko dawa ya Mtume Mohamed (mkojo wa ngamia) ?

29. Mtume Mohamed alisema kwamba kula matende saba kila siku inakinga mwili barabara. Lakini kama matende haya yana asenia, risini na kemikali nyingine, je yangali yanafaa ?

30. Waislamu wengi husema kwamba Kuran ni kitabu kilichojaa uvumbuzi na sayansi. Kwa nini Waislamu hawakuvumbua kompyuta, televisheni, vyombo vya kusafiri angani, chanjo, friji, dawa za viuavija, na kwa nini wako nyuma katika sekta zote za sayansi, mathalan katika kusoma muundo wa vinasaba ? Waislamu ambao wanadai kuwa na « kitabu hicho cha sayansi » watatuletea usomi gani kuhusu kutatua matatizo ya kuongezeka kwa hewa ukaa na kupanda kwa halijoto duniani ?

31. Mtume Mohamed anasema kwamba aina ya kisibiti cheusi kinatibu kila aina ya maradhi. Je, dawa hiyo ina uwezo wa kutibu ukimwi, kisukari, ukoma, tende na kadhalika ?

32. Waislamu wengi husema kwamba Mtume Mohamed ametajwa katika Biblia. Lakini si wanasema pia kwamba Biblia imepotoshwa ? Haieleweki.

33. Katika Waislamu hawa wengi wanaosema kwamba Mtume Mohamed ametajwa katika Biblia, je wanajua kwamba Kuran haijasema vile ?

34. Wasomi wengi maarufu wa Kuran kama Ibn al-Layth, Ibn Rabban, Ibn Kutayba, Al-Ya'Kubi, Al-Tabari, Al-Bakillani, Al-Mas'udi na Al-Bukhari wamethibitisha kwamba kitabu kitakatifu Taurati hakina dosari wala hitilafu. Je, kwa nini Waislamu wengi wa siku hizi hawawasikii ?

35. Endapo Biblia ni kitabu ghalati, kwa nini Allah hakuwasaidia Wakristo wasikipotoshe kitabu chao ?

36. Iwapo Waislamu wengi waamini kwamba Allah alitaka kuwajaribu Wakristo na Wayahudi wa enzi zile, je kwa nini Waislamu wanaendelea kuamini Kudr’a ya Mwenyezi Mungu ? Hizo si itikadi kinzani ?

37. Inaaminika kwamba Kuran ilishushwa kwa ajili ya wanadamu wote. Kwa nini Kuran haizumgumzii dini nyinginezo kama zile za Budda, Hindu na Tao ?38. Inasemekana kwamba Allah hupendelea kupiga chafya kuliko kwenda miayo wakati ni wazi, kwa mujibu wa sayansi za kisasa, kwamba kwenda miayo ina faida nyingi kuliko kupiga chafya ? Si chafya zile zinachangia kusambaza viini vya maradhi ?

Maoni 13 :

 1. Mwalimu Pascal Bacuez

  Nilisoma makala hii siku ile ile ulipoichapisha. Tunazihitaji makala za namna hii, zinazochangamsha akili. Baadhi ya masuala yaliyomo nami yamenitatiza kwa muda mrefu. Mfano ni hili suala la uhuru na haki ya binadamu ya kuwa muumini wa dini aitakayo. Tangazo la kimataifa la haki za binadamu linaitambua haki hiyo. Mtu ana uhuru na haki ya kuwa na dini au kutokuwa na dini. Ana haki ya kubadili dini.

  Lakini nimeona kuwa wa-Islam wanaotaka kuihama dini hiyo wanatiwa msukosuko, hata kutishiwa maisha yao. Mifano iko, kama vile Wafa Sultan (mzaliwa wa Syria), na Ayaan Hirsi Ali (mzaliwa wa Somalia).

  JibuFuta
  Majibu
  1. Asiyejulikana28/6/16

   Uislamu haumlazimishi mtu kuingia wala haumkatazi mtu kutoka. Hili liko wazi. Watu wanaotoa vitisho kwa watu wengine ni jambo la kawaida tu hata kwa wanasiasa. Lakini hawana authority ya kumtisha mtu. Uislamu unaamini kuwa Allah ndie atakaewalipa binaadamu kwa matendo yao.

   THERE SHALL BE no coercion in matters of faith.- 2:256 (Asad)

   Futa
  2. Shukrani sana kwa mchango wako. Natumaini kwamba maoni yako ndiyo yanayozingatiwa na waislamu wote duniani. Lakini tunajua kwamba sura uliyotaja hapo (2-256, ambayo maana yake ni : hapana ruhusa kumlazimisha yeyote kuingia katika dini) ni sura ambayo imefutwa au kurekebishwa na sura nyingine (9-29) ambayo ilishushwa baadaye wakati Mtume Mohamed alipokuwa ameshahamia Madina. Na zipo nyingine kama hizi zifuatazo : 5-33 ; 3-90 ; 16-106 na 4-137.

   Isitoshe kuna hadith mbili za Sahih Al Bukhari (6484) na Sahih Muslim (1676) ambazo kwa kweli zinazingatia dhana kinzani inayopingana na aya ile uliyoitaja.

   Futa
  3. Mimi naona kinachosumbua watu ni hukumu ya kuuawa kwanza na pili kwa 'kosa' la kubadili dini. Niwaulize Prof Mbele na Pascal, je nyinyi mnaamini juu ya usahihi wa hukumu ya kifo kwa mujibu wa dini zenu au sheria za nchi zenu?

   Futa
 2. Asante Prof Mbele kwa ujumbe wako. Nimefurahi kuona kwamba tunakwenda sambamba katika kuhoji masuala haya ambayo licha ya kutukanganya sisi ambao tunasoma sana, yanatatiza pia wengi katika dini hii ya kiislamu. Wengi wanaotoka katika dini hii wanaishi katika hofu kubwa. Kwa bahati mbaya, tangazo la kimataifa la haki za binadamu halina ufanisi wala uhalali katika nchi nyingi za kiislamu. Mbali na Wafa Sultan na Ayaan Hirsi Ali, wengi wenye ujasiri mkubwa wanaanza kusema na kuandika maandishi ya kufikirisha kama yale ya Waleed Al-Husseini, Boualem Sansal na kadhalika. Tamaa ipo.

  JibuFuta
 3. Mwalimu Bacuez,

  Shukrani. Ili kusaidia kusambaza ujumbe wako na kuhamasisha mjadala, nimeuongelea katika blogu yangu.

  JibuFuta
 4. Maswali yako ni ya msingi, tekenyeshi kifikira na fikirishi. Hata hivyo, umesahau swali moja muhimu ambalo ni kwanini Mohamad aliacha Quran bila kuandikwa; na ikaandikwa baadaye? Je hawa walioiandika hawakuingiza mambo yao au nao walikuwa wamevuviwa kama wasemavyo watetezi wa Quran? Je hawa walioandika Quran na Mohamad ambaye aliiacha bila kuandikwa tumwamini nani na kwanini? Hili la vigori na kutoheshimu haki za binadamu liko wazi kabisa. Uislam sawa na Ukristo ni dini kandamizi zinazowadhulumu akina mama, watu weusi na wasio waislam kwa ujumla. Quran ilikuwa na maana sana kwa watu wa wakati ule lakini siyo sasa. Mfano mdogo ni kwamba waislam huchukulia msalaba kama alama ya laana jambo ambalo ni kujipinga hasa ikizingatiwa kuwa ndege wanazotumia kwenda Makka zina umbo la msalaba huo huo wanaoulaani ukiachia njiapanda nyingi wanzovuka au dari za nyumba zao. Kuhusu utakatifu wa Makka nao ni shaka tupu. Mungu anayesema Makka ni patakatifu kuliko Afrika atakuwa na matatizo hasa ukizingatia suluba za jangwa kama Saudia. Nimeishatoa mchango mwingine kwenye blogu ya ndugu Mbele kwa ufupi japo. Kuhusu sayansi, hili liko wazi. Uislam na Ukristo hauna tofauti kwenye umbumbumbu wa sayansi. Jikumbushe kisa cha kutishiwa maisha kwa mwanasayansi wa nyota na mwanafalsafa na mwana mahesabu Galileo Galilei alipodai dunia huzunguka jua na si kitovu cha anga na sayari zote. Kwenye kitabu changu cha Africa Reunite or Perish nilijenga hitimisho kuwa dini za kimamboleo ni nyemelezi na koloni hasa ikizingatiwa namna zilivyotukana mila zetu na kutusingizia lakini hapo hapo zikataka tuheshimu uongo wake wa wazi. Suala jingine ni kwamba bila Biblia hakuna Qurani kwani Quran ni sehemu kubwa ya biblia iliyoandikwa kishairi. Angalia asili ya dhana za uumbaji, waumbwaji, namna ya uumbaji na ukuu wa Allah ambaya naye ukimchunguza sana utakuta asili yake ni Misri na si Uarabuni.

  JibuFuta
  Majibu
  1. NN Mhango, juu ya Qur'an na uandishi wake tulishajadili jambo hilo kwa urefu katika safu ya Prof.Mbele. Kama kunajambo ambalo hata weledi wa Qur'an wasiokuwa waislam hawajapatapo kutilia shaka ni uaminifu wa wale walioikusanya na kumalizia kuiandika Qur'an kuwa katika kitabu kimoja. Si kweli kuwa ya Qur'an haikuwa imeandikwa wakati wa Mtume s.a.w. Ni uwongo wa wazi! Twaweza jadili kiasi au sura gani zilikuwa zimeandikwa na sura gani zilikuja kuandikwa baada yake.

   Pili, Hayo maswali ya huyo alienda katika Ukristo baada ya kusilimu yote yanaakisi ni kiwango gani cha uelewa mdogo aliokuwa nao bwana huyo na bahati mbaya kwa kukosa kufanya utafiti au kuuliza wanavyuoni akafikia uamuzi huo. Yote ni maswali mepesi japo kuwa ni muhimu na yanajibika bila taabu yoyote. Nikipata wasaa nitayajibu moja baada ya jingine, In shaa Allah.

   Tatu, hizo tuhuma za nafasi ya msalaba kama laana katika Uislam ndio kwanza nazisikia kwako. Msalaba ni ishara ya Ukristo haina maana yoyote zaidi ya hapo katika Uislam. Hata The Encyclopædia Britannica kinasema kwamba msalaba ni “ishara kuu ya dini ya Kikristo.” Na kwamba baadhi ya Wakristo hawatumii msalaba katika ibada. Kwa nini? kwa sababu imeandikwa katika biblia sio Qur'an kuwa: ‘Amelaaniwa kila mtu aliyetundikwa juu ya mti.’” (Wagalatia 3:13). Mhango usitusingizie tafadhali, kuwa mkweli, unaweza ukapenda dini yako ya asili lakini usisingizia dini za watu yale ambayo hayapo. Si uungwana.

   Nne, vitabu vya dini na sayansi. Vitabu vya dini si vya sayansi japo mambo ya kisayansi yametajwa humo na katu huwezi linganisha Qur'an na Biblia au dini yako ya asili katika umahiri wa kuyaeleza mambo ya kisayansi kwa usahihi. Msome Mwanasayansi Dr. Maurice Bucaille katika kitabu chake "The Bible, The Qur'an and Modern Science." Hayupo peke yake, wanasayansi kadhaa wamebadili dini na kufuata Uislam, baada ya kukinai kuwa Qur'an ni maneno ya Mungu. Hayo yaliomkuta Galileo katika himaya ya Ukristo, hata siku moja hatosikia katika Uislam. Waislam hawajapatapo hata kusingiziwa juu ya kuhatarisha maisha ya wanasayansi.

   Tano,dai kuwa 'bila Biblia hakuna Qurani' nilishakujibu jambo hili sehemu nyingine. Sioni haja ya kurejea hapa zaidi ya kusema tu kuwa kitabu chako kwa hitimisho hilo kimeongeza idadi ya vitabu ambavyo mimi huvipa grade F yaani Failure.

   Futa
 5. Kwanza nikushukuru sana kutuletea mchango wako mwenye maana hapa penye blogu hii.

  Pili naomba nikusisitizie kwamba maswala hayo yote yameletwa na rafiki yangu Yusuf wala si ya kwangu. Mengine hayana noma kama tunayachukulia yalivyo lakini mengine yanarejelea imani yake Yusuf mwenyewe. Binafsi naiheshimu ingawa nina mushkeli nayo. Mfano ni tanzil (kushuswa msaafu wa Kuran) kwa waislamu ni imani kama ilivyo utatu kwa wakristo. Yusuf anaiponda imani hiyo ilhali si haki, vinginevyo waislamu wenyewe wangekuwa na haki ya kuiponda imani ya utatu kwa kujidai kwamba wanajua kuikosoa na kuisahihisha. Jambo ambalo haiwezekani kwa sababu imani haikosoleki.

  Hivyo basi, licha ya kuwa ni imani kwanza, dini yoyote pia ni maandishi, utamaduni, majengo, fasihi, siasa, sheria, tambiko, kaida, visasili na kadhalika. Hapo ndipo sisi wanadamu tunayo haki ya kuikosoa dini ya aina yoyote hasa wakati dini hizo huenda tenge. Na mbinu za kuihakiki dini tunazo ikiwa ni pamoja na akiolojia, ipigrafia, filolojia, uhakiki mbalimbali ya nyaraka za zamani, historia na kadhalika. Mfano mzuri ni zile nyaraka zilizogunduliwa mwaka 1972 Yemen katika mji mkuu Sanaa. Na tunajua sasa kwamba hizo nyaraka ni dondoo mojawapo ya Kuran ambazo zimeleta maono mapya juu ya Kuran jinsi ilivyohalilishwa chini ya utawala wa Kalif Uthman. Hivyo utafiti na uhakiki wa Uislamu unaendelea.

  Kuhusu Ukristo, usisahau kwamba Afrika ni janibu ya kwanza duniani iliyofikwa na Ukristo karne ya nne katika Ufalme wa Axum Ethiopia, kwa hivyo kabla ya Ukristo ulipofikia Ulaya. Na hadi leo, Ukristo huo umejenga utamaduni mkubwa sana : majengo, liturjia, matambiko na maandishi ya kiajabu (yenye kutumia alfabeti ya kienyeji itwayo G’ez).

  Sidhani kama — lakini nitakiri kujirekebisha — tutanufaika katika kutafakari na kusaili dini ya Ukristo na Uislamu huku tukichanganya dini hizi mbili. Kwa kifupi, naona kwamba kweli Ukristo (lakini kama asasi zote za kibinadamu) ilikuwa ni dini kandamizi (kama ulivyoandika) lakini kihistoria Ukristo ulikuwa mkatili kwa kadiri ilivyoacha kusoma Biblia wakati Uislamu unaelekea kuwa na uhayawani mkubwa kadiri unavyozidi kubobea katika kusoma maandishi yake matakatifu.

  La mwisho hapo, maadamu umetaja vitabu vyako, nitapendezewa “kuvivinjari” ikiwa vinapatikana kwa njia rahisi. Asante.

  JibuFuta
  Majibu
  1. Pascal, mimi nisingekujibu kama usingetumia lugha ya matusi na kunasibisha na Uislamu. Umedhihirisha kukosa uungwana na nidhamu ya mjadala. Ni kweli huwezi changanya dini hizi mbili au yoyote nyingine. Wakati unakiri kihistoria Ukristo kuwa mkatili kadiri ulivyoacha kusoma Biblia, hebu tuanzie hapo je kuna mambo ya kuchefua roho kama yaliomo katika biblia? Hebu anzia hapa; https://callingchristians.com/2011/12/23/29-sexually-explicit-profane-and-dirty-stories-and-verses-in-the-bible/

   Pili, hebu tuthibitishie 'Uhayawani' wa Uislam (Qur'an) kwa kadri uwezavyo. Tujadili.

   Futa
  2. Pascal hana haja ya kukujibu kwa vile nawe umetumia hasira na kukosa ustaarabu huko huko unakomshitakia. Hujui kuwa bila biblia, kurani haina lolote wala maana? Sijui kwanini watu wanapenda kuona mabaya ya wenzao wakati wakifumbia macho yao. Dini nyemelezi za kigeni haziwezi kutetewa hata kwa jazba na matusi. Ukristo na Uislam ni dini ya hovyo zilizoletwa Afrika kutukana mila zetu na kueneza uongo na majisifu wakati hazina tofauti na dini zetu asilia. Mwenye kujifanya dini yake ni bora kuliko zote basi amwambie huyo muungu wake akijitokeze tumuulize maswali hasa ikizingatiwa asili ya dini za kiafrika ni kwamba Mungu wake haonekani wala hajigambi kama hii miungu mamboleo.

   Futa
 6. Mwalimu Bacuez nakushukuru sana kwa majibu yako yasiyolalia popote. Kimsingi, tunatofautiana kitu kimoja. Mimi nakwenda mbele na kupendekeza hizi dini zifikishwe mahakamani kwa unyama ziliotenda hasa kuvuruga historia yetu, kutusingizia, kutuibia kupitia ukuwadi wa kikoloni na biashara ya utumwa. Sipendi wala kuukubali udugu unaohubiriwa sasa baada ya waswahili kuuzwa. Vitabu vyangu vinapatikana Amazon na kimojawapo cha AFRICA REUNITE or PERISH unaweza hata kusoma kwenye google scholar. Nashauri wanazuoni tushikie bango kuumbua mila za watu zinazoitwa dini wakati nasi tulikuwa na dini zetu tena zenye kuthamini utu kiasi cha kutotushawishi kwenda kuwatawala wengine kama tulivyofanyiwa. Ni leo tu nimewasilisha mswaada wa kitabu kingine cha The need to decolonise and detoxify education: Doing away with colonial legacies embedded in the current dominant grand narrative.
  Nashukuru kwa mchango wako hasa kuleta haya maswali ya Yusuf muathirika wa dini zote mbili. Kimsingi ameonyesha kuchanganywa na dini husika.

  JibuFuta
 7. Ndugu Khalfan Abdallah Salim

  Nimesoma taarifa uliyoleta, hii hapa, inayoelezea mambo ya ovyo yaliyomo katika Biblia. Nimeona inasisimua, kwa jinsi ilivyoelezea mambo ya wanadamu. Wala siwezi kupandisha jazba kwa kuwa watu wameifukua Biblia wakaanika hadharani mambo yaliyomo.

  Binafsi, mtazamo wangu ni kuwa tusome misahafu kwa kutumia akili tuliyo nayo na kuchambua tunayosoma. Tusiisome kikasuku. Kuna mambo katika hii misahafu ambayo si ya kufuatwa na wala hayatufai. Kwa mfano, katika Biblia na katika Qur'an, utumwa unaongelewa kama vile ni jambo la kawaida kabisa, linalokubalika. Watumwa wanatajwa katika Biblia na katika Qur'an bila kuhoji kama suala zima la utumwa ni halali au la. Hakuna hata dalili kuwa watumwa ni wanadamu kama wengine, wanaostahili kuwa huru.

  Leo watu tuna akili na mtazamo tofauti. Tuna ufahamu wa haki za binadamu. Tunapinga utumwa. Kwa hivi, ni lazima tupinge msimamo wa Biblia na Qur'an kuhusu utumwa. Hapo hakuna sababu ya kudai kuwa msahafu ni neno la Mungu, na kwamba ni marufuku kubadilisha chochote. Kudai kwamba msahafu ni neno la Mungu ambalo halipaswi kubadilishwa kwa vyovyote ni mtazamo wa hatari.

  Nitoe mfano mwingine, kuthibitisha umuhimu wa kutumia akili tuliyo nayo leo katika kusoma misahafu. Katika u-Islamu na u-Kristu kuna mafundisho yanayohimiza kuwasaidia maskini. Katika u-Islam hiyo ni nguzo mojawapo, yaani "zakat," kati ya nguzo tano. Sasa, tusipotumia akili yetu ya leo, ni lazima tutakwama. Suali ni je, tukijenga mfumo wa jamii wa haki na fursa kwa wote, tukafuta umaskini, tutakuwa tumekiuka mafundisho ya dini? Tukiondoa umaskini hapa ulimwenguni, tutakuwa tunapinga nguzo ya u-Islam ya "zakat"? Naona itabidi u-Islam ubaki na nguzo nne badala ya tano.

  Hayo ni aina ya masuali tunayopaswa kujiuliza kwa kutumia akili tuliyo nayo leo. Hatuwezi kung'ang'ania kuwa tufuate kila kilichoandikwa katika Qur'an au Biblia au msahafu mwingine wowote. Lakini, kama tunavyojua, mtu ukijenga hoja kama hii ninayojenga, lazima utakumbana na jazba za wale wanaodai kuwa msahafu haupaswi kubadilishwa hata chembe.

  JibuFuta